Na Carren Omae Kufuatia madai ya Ufisadi ambayo yameanza kumwnadama Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi Philip Kinisu, amesema hatojiuzulu. Akiwahutubia wanahabari Jumanne asubuhi, Kinisu amesema iwapo atafanya huenda kuna watu ambao wakatumia njia za kutoa madai kuwashinikiza maafisa wa serikali kujiuzulu nyadhfa zao. Amesema kuna watu wenye ushawishi na ambao wanachunguzwa na EACC na ambao wameanza kutumia madai hayo kukandamiza uchunguzi dhidi yao. Suala hilo linahusiana na malalamishi yaliyoibuliwa na Shirika moja kwa jina Bunge la Wananchi, ambao walilalamika kwamba kampuni moja inayohusishwa na Kinisu ilihusika katika biashara ya mamilioni ya pesa na NYS , ambayo inachunguzwa na EACC inayoongozwa na Kinisu. Hata hivyo Kinisu amesema kampuni hiyo ilianza kufanya kazi kabla yake kuteuliwa katika wadhfa anaoushikilia sasa huku akisema suala hilo linachunguzwa na idara kadhaa na wala sio EACC pekee. Tayari, EACC imetangaza kwamba kundi la wataalam linashughulikia malalaishi yaliyoibuliwa dhidi ya Mwenyekiti wake huku Kinisu akisema yuko tayari kushirikiana na wachunguzi.