Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Binadamu limeelezea wasiwasi kuhusu ghasia ambazo zimeripotiwa humu nchini.
Katika taarifa yake leo hii Shirika hilo limetoa wito kwa uchunguzi wa wazi kufanyika kuhusu madai ya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya waandamanaji.
Shirika hilo limesikitikia ripoti kwamba takriban watu ishirini na watatu wamefariki dunia kufuatia visa hivyo likitaka watakaopatikana na hatia kuchukuliwa hatua.
Kuhusu maandamano ambayo yamepangwa na Azimio Juma lijalo, limezitaka idara zinazohusika kuhakikisha kuwa maandamano yenyewe yanakuwa ya amani na kwamba hakuna watu watakaojeruhiwa au hata kuuliwa.
Kwingineko, Shirika la Umoja huo wa Mataifa linalowashughulikia Watoto UNICEF vile vile limeelezea hofu kuhusu usalama wa watoto kufuatia ghasia ambazo zinaendelea kushuhudiwa.
UNICEF imesema kuna haja ya mikakati kuwekwa kuwalinda watoto wakati wa hali kama hizi.
Ikumbukwe Jumatano wakati wa maandamano ya Azimo takriban wanafunzi hamsini na watatu wa Shule ya Kiumbuini iliyoko Kangemi hapa jijini Nairobi walilazwa hospitalini baada ya polisi kuwarushia vitoza machozi.