Na, Beatrice Maganga Masaibu yanaendelea kumwandana aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi, Ann Waiguru baada ya Bunge la Kitaifa kuidhinisha ripoti ya Kamati ya Uhasibu wa Umma, PAC inayopendekeza Waiguru azuiwe kuwania wadhifa wowote wa umma kutokana na sakata ya ufujaji wa fedha katika Taasisi ya Kitaifa ya Huduma za Vijana, NYS iliyokuwa chini ya usimamizi wake. Ripoti hiyo iliyoandaliwa na PAC chini ya uwenyekiti wa Mbunge wa Rarieda, Nicholus Gumbo vilevile inapendekeza Waiguru afanyiwe uchunguzi kuhusu mali aliyomiliki katika kipindi alichokuwa Waziri wa Ugatuzi. Ripoti hiyo inapendekeza kwamba azuiwe kuwania wadhifa wa umma iwapo atapatikana na hatia ya ufujaji wsfedha za umma.
Takriban shilingi bilioni 1.2 zinadaiwa kufujwa kupitia miradi mbalimbali ya NYS wakati wa utawala wa Waiguru. Ripoti hiyo ambayo ilipigwa msasa na bunge kabla ya kuidhinishwa leo vilevile inapendekeza kampuni ya uanasheria inayohusishwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen ichunguzwe kwa madai ya kupokea kima cha shilingi milioni kumi na tano kutoka kwa kampuni moja inayohusishwa na sakata ya NYS.
Aidha inapendekeza kuchunguzwa kwa Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Dkt Partrick Njoroge pamoja na maafisa wengine kuhusu madai kwamba walichangia kufujwa kwa fedha za umma kwa kutozuia uhamisho wa mamilioni ya fedha kutoka kwenye akaunti za Wizara ya Ugatuzi hadi kampuni kadhaa zilizopewa kandarasi mbalimbali. Katika ripoti hiyo jukumu kuu limepewa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, Idara ya Upelelezi na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ili kuchukua hatua zifaazo.