×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Nani atakuwa wa kwanza kuwajibika 2016

Living

Tumeingia msimu wa kujiuliza maswali mengi huku mwaka mpya ukikaribia, huu ni kwa mujibu wa dini ya ndugu zangu wakristo.

Huu ni msimu wa kupendana, kusheherekea na kuwa mamoja mbele ya mwenyezi Mungu. Ni msimu wa kutoa na kusameheana.

Swali langu ni, nani yuko tayari kumsamehe mwenzake? Je, kuna aliyetayari kuregesha mali ya wizi? Kunaye aliyetayari kuwahudumia wakenya pasi na misingi ya dini, kabila na ufisadi?

Bila shaka mwaka wa 2016 utashuhudia mijadala na mipango makhsusi ya kila mmoja kutaka kuanza kufungua ukurusa wa maisha yake upya. Kuna wale walioapa kuacha kuvuta sigara, kunywa pombe, kuoa au kuolewa, kununua gari, kusafiri miongoni mwa mambo mengine mengi.

Kati ya maono zao zote ni vigumu kupata mtu akisema kuwa mwaka wa 2016 utakuwa mwaka wa ibada kwake, utakuwa mwaka wa kuangalia mayatima, utakuwa mwaka wa kuongeza vyumba vya ibada na kuwasaidia maskini. Hakika binadamu ni mtu ovyo sana mbele ya Mungu.

Kila mara yeye huweka maslahi yake mbele na kumkumbuka Mungu pale anapopata shida. Wakenya wenzangu leo hii najua wengi watashangazwa na mjadala wangu wa wiki hii kwani wengi wamezoea mijadala yangu nyeti ya kupiga na kuvua.

Ujumbe wangu kwa wakenya tarehe ya leo ambayo ni siku muhimu kwa ndugu zangu wakristo ni moja tu! Abuduni Mungu badala ya miungu midogo midogo, jiondoeni ndani ya makabila na mfuate kabila la Mungu na mafundisho yake?

Wengi wetu nyoyo zao chafu kama pipa kwa sababu ya chuki za kikabila na kile ninachokitaja kama upumbavu wa hali ya juu unaotokana na utumwa wa kujitakia na kuamini kuwa siku haliendi sawa kama fulani hajasema.

Kwa kipindi cha miaka mitatu serikali ya jubilee kwa njia moja au lengine imewakosea wakenya. Ni katika kipindi hiki ambapo pesa za NYS, Eurobond, SGR, wizi wa ardhi, Chicken gate, miongoni mwa sakata zengine zimekuwa zikigonga vichwa vya habari.

Polisi nao wamekuwa kama maskauti wa kufuata amri za kitoto badala ya haki, wizara ya usalama wa ndani imejisahau na kuanza kuwatisha waandishi wa habari badala ya kukabiliana na adui wa taifa.

Wakenya wengi wamelemazwa na kuuawa kutokana na visa vya ugaidi na uhalifu wa kila siku. Naamini sote tumechoshwa na vituko vya mwaka huu.

Natumai mwaka ujao unafiki huu utapitwa na wakati. Natumai mwaka ujao badala ya kutoa maono ya kuiba zaidi wanasiasa wetu watatoa maono ya kuwasaidia wakenya, natumai wataregesha pesa zote walizoiba na kuomba msamaha kwa kuwafukarisha wakenya.

Leo hii wakenya wanaweza simama juu ya jukwaa na kunukuu baadhi ya vipengele vya katiba, misemo ya watu mashuhuri huku wakipigiwa makofi na kuonekana wasomi lakini wanapoambiwa watoe aya Fulani kutoka kwa Bibilia au Quran utawapata wakikodoa macho mithili ya mtu aliyekabwa koo na kiazi kimoto na hata kucheza na jina la Mungu kama kamari.

Tabia kama hizi ndizo zinazozaa maombi ya kila siku ya kuwaombea viongozi wezi, maombi yanayoongozwa na baadhi ya viongozi wa dini ambao sasa badala ya kuhubiri neno wanahubiri meno. Tulipofikia sasa ni hatari, na iwapo sote hatutajibadilisha. Maskini atakapokosa cha kula basi mkae mkijua chakula chake kitakuwa ni nyinyi matajiri wachache.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Similar Articles

.

Recommended Articles