Hassan Ali Jumapili iliyopita jioni punde baada ya kumaliza kupeperusha hewani Redio Maisha matangazo ya moja kwa moja pambano la ligi kuu ya Uingereza baina ya Chelsea na Leicester, nikapokea arafa ya msikilizaji wangu wa dhati, ashiki hasa, aitwaye Sammy Van Adura: “Hongera sana Hassan na mwenzio Mukangai kwa kutuletea mechi mbali mbali za ligi ya Uingereza, EPL, hadi msimu kufikia tamati. Twawatakia umri mrefu na mzidi kutuletea mechi kadha zijazo.” Ndugu Van Adura hujui ni kwa vipi uliugusa mtima wangu! Pamoja na kwamba ni kazi yangu kukutangazia, inapendeza zaidi nikijua kuwa msikilizaji wangu ameridhika kiasi hicho! Kutoka chini ya kipembe cha moyo wangu, leo hii nachukua fursa hii kuwahongera, kuwavisha pete na kuwazimia sigara wanahabari wenza wa michezo, hususan watangazaji wa mpira. Msimu wa ligi kuu ya Uingereza umefikia tamati. Leicester FC imewashangaza wengi kwa kulitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza kabisa katika historia yake tangu kuasisiwa miaka mia moja na thelathini na miwili iliyopita! Mwafrika wa kwanza kutoka nchi ya Algeria Riyad Mahrez akaweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka bara hili kutuzwa mwanandinga bora! Usisahau kuwa kinyozi wake ni Mkenya kutoka Pwani, Bw. Najim! Na kama wasemavyo watu visiwani Zanzibar ni kuwa kukamilika kwa safari ya leo ni maandalizi ya safari ya kesho. Watangazaji wa kambumbu nchini – hasa redio – tunasubiriwa kwa hamu kubwa wikiendi ijayo fainali ya klabu bingwa barani Ulaya (Real Madrid dhidi ya Atletico Madrid, (Madrid Derby) uwanjani Giuseppe Meazza nchini Italia. Kisha Juni twasubiriwa kwa fainali za Uro nchini Ufaransa. Watangazaji wa kabumbu redioni hongereni sana. Hongera hizi sio tu za kukuza lugha tukufu ya Kiswahili kupitia kwa matangazo ya moja kwa moja, lakini pia kuleta burudani katika familia na utangamano kwa ujumla nchini. Ndio, wapo wanaotushtumu baadhi yetu kwa kuboronga lugha, lakini ikumbukwe kuwa hakuna binadamu mkamilifu. Hakuna mjuzi wa wajuzi ela Mola pekee. Siye tuko tayari kujifunza. Lakini si kwa masimango jamani. Leo hii watangazaji wa mpira wanatagaza katika mazingira magumu ya ushindani. Runinga zi tele sikwambii vibandani. Zama zao kina Leonard Mambo Mbotela, James Abilla, Stephen Mwita Koroso, mwendazake Billy Omalla Mchanji, marehemu Nick Okanga Naftali, Salim Mohammed, Mohammed Juma Njuguna, Ali Salim Mmanga, Jack Oyoo Sylevester, Ismael Mohammed na wengineo (wazee wetu waliotutangulia), kulikuwa na runinga moja kijijini. Hivyo wengi walitegemea sana redio. Hapo ungehadaa. Angefunga goli Seif Mutie na ukosee kwa kutaja John Odie! Hizi ni zama za utangazaji na uchanganuzi wala sio anakwenda anakwenda goooli pekee! Leo hii! Subutu! Simu. Mitandao. Idhaa mbali mbali za redio. Sijakwambia “wawekezaji’ wanaobeti. Wanazijua hata timu za daraja la tatu nchini Kazakhstan! Hassan mwana wa Ali, Stephen Mukangai mwana wa Norah, Michael Were Mukhusia aka Bonga Boli, Diblo Kaberia Elmago, Fred Arocho aka Twiga, Japheth Kahindi Makanaki, Kaka Zema, Beki wa kupanda na kushuka Geoffrey Mwamburi, Jacob Icia, Rashed Abdallah, George Waka,… Orodha ni ndefu. Pongezi sana kwa kukuza Kiswahili na kuupa ubongo burudani wenzangu. Taratibu tutafika! Ipo siku… Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA). [email protected], [email protected], FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali, Twitter: @alikauleni
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media
platforms spanning newspaper print
operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The
Standard Group is recognized as a
leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national
and international interest.