×
App Icon
The Standard e-Paper
Truth Without Fear
★★★★ - on Play Store
Download Now
×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Mohammed Ali's Jicho Pevu: Ni Huduma ama Dhuluma Centre?

Living

Naandika nikiwa na wingi wa machungu ya jinsi Huduma Centre na vituo vyote vya uandikishaji wa vitambulisho vinatumiwa na baadhi ya genge la wakabila kuwadhulumu baadhi ya Wakenya wanaonekana kutoka mrengo wa upinzani na Waisilamu kwa jumla.

Jumba hili sasa si la huduma kwa Wakenya, ila huduma za kuandikisha idadi kubwa ya vitambulisho kwa wafuasi wa Jubilee ili waweze kufaulu kupiga kura mwaka wa 2017 na kuwanyima Wakenya wengine fursa ya kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba.

Nasema haya kwa sababu dadangu ni mmoja wa wale waliodhulumiwa na huduma centre hii ya dhuluma kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja sasa. Baada ya kumaliza shule yake ya upili mwaka jana kama Wakenya wengine, alielekea katika kituo cha kitambulisho cha Thika licha ya changamoto alizopitia za kuangaliwa na jicho la ugaidi, Muislamu na mpinzani wa serikali hatimaye alijisajili tarehe Januari 19, 2015.

Lakini hadi leo, dadangu hana kitambulisho licha ya kuwa mwanafunzi katika chuo kikuu. Hana raha, hatoki kama Wakenya wengine kwa sababu ya kusumbuliwa na polisi. Hawezi tekeleza huduma zozote kwa sababu hana kitambulisho cha kufanya hivyo, hawezi safiri kwa sababu Huduma Kenya imefanya maisha yake kuwa ngumu, kando na kumfanya mtumwa ndani ya nchi yake. Hii ndio huduma ya chuki inayoenezwa na takriban huduma zote nchini.

Ukiwa Muislamu Kenya ni hatia, kupewa kitambulisho lazima watengwe; kupewa pasi ya usafiri vivyo hivyo. Je, hii kama sio huduma mamluki ni nini? Mwaka uliopita, mtoto wangu aliyekuwa na umri wa miezi sita alitakiwa ajisalimishe katika jumba la Nyayo ili apewe fursa ya kuhojiwa kubaini iwapo ni Mkenya!

Katika jumba hilo, Waisilamu wengi wamedhalilishwa na kutengwa kando ili wapewe huduma hiyo. Hii si Ukenya, hii ni ubakaji wa haki na msingi ya Wakenya kuishi. Majuzi kiongozi wa upinzani Raila Odinga alianzisha kampeini ya Wakenya kupewa vitambulisho baada ya vilio kutoka kwa baadhi ya Wakenya.

Enyi wana Huduma Centre, tumechoka na huduma zenu za kikabila. Kama mwataka kuwashughulikia Wakenya chini ya mwamvuli wa Huduma Kenya, basi wapatieni vitambulisho bila ya kuangalia kabila zao. Kenya itasimama imara kupitia maamuzi ya Wakenya.

Utaifa tulionayo hautaturuhusu kufyatua domo wakati mambo yanapokwenda kombo. Enzi za ujahilia za Kanu zimepitwa na wakati, enzi za kuwalazimisha watu kuabudu miungu imepitwa na wakati, enzi za utawala wa ki-imla kupitia maafisa wa serikali zimepitwa na wakati.

Ufisadi, dhuluma na ukiukaji wa haki vimekuwa kama chakula serikalini, huku vitu kadhaa vya serikali vikitumiwa kuendeleza sera hi chafu ya mtu mle mtu.

Mwahubiri Ukenya na huduma bora ilhali baadhi yenu mnatumiwa na wakabila wenzenu kuponda uhuru na haki ya Wakenya. Mnazungumzia uzalendo mkiwa na hila za kinafiki, hila za kukandamiza demokrasia iliyopiganiwa na watangulizi wetu.

Enyi wanafiki mnaodhalilisha Wakenya, jueni zenu pia zitafikia mwisho. Kenya haina mwenyewe, Kenya ni ya Wakenya. Vitambulisho tutapata tu hata kama tutavumilia kwa muda. Udhalimu wenu wa kutenga Waisilamu na jamii zingine zitaisha siku moja. Mkumbuke sio wote walio na fikra chafu za kikabila kama baadhi yenu hapo Huduma Centre, wengine ni wangwana walio na mapenzi kwa Wakenya wenzao na wanaotoa huduma hizo pasi na misingi ya kikabila.

Jifunzeni kuwa na utaifa na kuhudumia Wakenya bila jicho la chuki linalozidi kukuzwa na baadhi ya genge la wanasiasa. Mambo ya kutenga Waisilamu kwa misingi ya kigaidi na kuita baadhi yao majina kama ‘Waria,’ ‘Watu wa Border’ na kunyima kabila zingine vitambulisho, haitawafanya mashujaa, ila wabakaji wa haki.

Sina raha kila nikipita mbele ya jumba hilo ambalo sasa limegeuzwa na kuwa jumba la kikabila. Ni aibu kila mara ninapoliliwa na Wakenya wanaozidi kuteseka kupewa haki yao na jumba hilo la kikabila. Natamani nijue ni nani huyu aliyetoa amri za kihayawani za kuwanyima Wakenya haki zao.

Natamani kujua ni mkubwa gani huyu mkabila anayeshuhudia haya yote bila kuchukua hatua za dharura. Natamani nimweleze hio si haki mbele ya Mungu, lakini kila mara ninapoona vile serikali inazidi kutuzamisha na kujipiga kifua eti itatawala hadi mwaka wa 2027, basi najua ni kwa nini wana imani ya kututawala kwa mabavu. Wakenya wamechoka na punda mrusha mateke. 

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected][email protected]; FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali; Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Trending Now

.

Popular this week

.

Similar Articles

.

Recommended Articles