×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Kunani Rio, Brazil jamani?

Living
 Kenya yetu jamani! Kunani huko Rio Brazil? Picha: Hisani

Ni joto la Olimpiki. Joto ambalo kwamba kwa muda sasa limefukuza kibaridi katika jiji la Nairobi na miji mingineyo nchini. Joto ambalo latifuliwa nchini Brazil na kuacha vumbi jingi tu nchini!

Kabla ya kulitathmini joto la Rio, hebu mwanzo tuwahongere wanaotamba huko Brazil. Sio tu ushindi wa dhahabu, fedha na shaba, lakini pia historia inaandikwa na rekodi kuvunjwa! Hapo sasa patamu! Pa rekodi kuvunjwa na historia kuandikishwa!

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya mashindano ya olimpiki Kenya ilijinyakulia medali ya dhahabu katika mbio za marathon. Jumapili tarehe 14 Agosti, 2016, kamwe haitasahaulika. Nalo jina la mshindi halitoweza kufutika aswilani katika mafuvu ya bongo za Wakenya.

Mwanadada Jemima Jelagat Sumgong. Alitima Jumapili hiyo katika muda wa saa mbili, dakika 24, sekunde 4. Ewe! Hongera sana da’ Sumgong! Ama kweli hapa Nairobian twakuvulia kofia Jelagat.

Mwengine wa kuzimiwa sigareti ni mshindi wa dhahabu mbio za mita 100, alfajiri kuamkia Jumatatu tarehe 15, Agosti, 2016. Mjamaika Usain Bolt. Bolt amelitakasa jina la riadha duniani ambalo linazongwa na kashfa za utumizi wa pufya, kwa kutimka muda wa sekunde 9.81.

Usain St. Leo Bolt, OJ, CD, mwenye umri wa miaka 29, ameshiriki mashindano yake ya mwisho ya Olimpiki kwa kutwaa dhahabu kama alivyofanya mwaka 2008 huko Beijing na 2012 London.

Tunaye pia Mwingereza Michael Fred Phelps II. Hadi tunapoyaandaa makala haya, Phelps alikuwa ametijilia mkwijini jumla ya medali 23 za dhahabu katika awamu nne za makala ya Olimpiki ambazo ameshiriki. Brazil pekee amechukua dhahabu sita! Yaani, mwanaraidha mmoja pekee anajinyakulia medali nyingi kiasi kwamba anayashinda mataifa zaidi ya mia dunian! Ebo!

Kivyovyote itakavyokuwa huko Rio, timu ya Kenya, chini ya wizara ya michezo itabidi kuwaeleza Wakenya kunani. Maswali mengi tu hayajajibiwa. Miye nitauliza tu haya:

Hivi mbona hatukumjibu kepteni wa kikosi cha Kenya mheshimiwa Wesley Korir, alipolalamikia maandalizi duni, ikiwemo ‘kufanyiwa sachi’ za utumizi wa dawa za kulevya kiholela? Nani ndiye aliyechelewesha jezi za mazoezi za Team Kenya?

Uteuzi wa timu ya uogeleaji mbona ulizongwa na mmmm? Kwa nini kocha wa raga kina dada, Lioness, alitaka kuachwa nyuma?

Ni ujumbe wa watu wangapi waliosafiri Rio, na kila mmoja jukumu lake ni lipi? Tiketi ya ndege ya Julius Yego kaificha nani? Na mbona kocha wake kutelekezwa?

Ni nani atatueleza ukweli kuwahusu watu hawa: Meneja Michael Rotich, na kocha John Anzra? Ati Rotich akihojiwa na kituo cha ARD/WDR cha Ujerumani na gazeti la Sunday Times alikubali kula pauni kumi alfu ili kuwaficha wanariadha watumiaji muku? Ati Anzra naye ‘alijifanya’ ndiye mwanariadha wa mbio za mita 800 Fergusson Rotich! Anzra mwenyewe akizungumza kwenye runinga ya KTN na pia kwenye Redio Maisha, alitoboa jipu! Ukimsikiliza utamhurumia mzee wa watu. Utajiuliza hadi lini jamani?

Waziri wa michezo Dr. Hassan Wario, Kamati ya Taifa ya Olimpiki Nchini, NOCK, Chama cha RiAdha nchini, AK, naomba tu kujua: KUNANI RIO, BRAZIL? Kenya yetu jamani! Kunani huko Rio Brazil?

Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).

[email protected], [email protected], FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali, Twitter: @alikauleni

Related Topics


.

Similar Articles

.

Recommended Articles