×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Kuna serikali kweli Kenya?

Living
 Photo:Courtesy

Miezi kadhaa iliyopita, profesa mtajika Makau Mutua alijitoa wazi wazi na kumkana Uhuru Kenyatta kama rais wake, licha ya kuwa Mkenya. Profesa Mutua alikuwa ameghadhabishwa na utendakazi wa serikali ya Uhuru. Wakenya walishangazwa na uamuzi huo wa mwananchi wa taifa lililojaa viongozi fisadi, taifa linalojiita taifa huru sio kwa Wakenya, bali kwa wezi wachache wanaobaka demokrasia.

Wakenya wenzangu, nimelifikiria jambo hili kwa muda sasa na kwa hakika, mimi pia naona nikiwakana viongozi wa nchi hii. Ndiposa leo nakupa sababu zinazonifanya ni hisi kana kwamba taifa hili si la kujivunia.

Vifo

Uongozi wa Jubilee utaingia katika vitabu vya historia kama uongozi ulioongoza Kenya kwa majeneza. Tangu Jubilee iingie mamlakani, Wakenya zaidi ya mia tatu wamepoteza maisha yao kutokana na hali mbaya ya usalama.

Vifo hivyo vilitokea baada ya mashambuliza ya kigaidi Westgate (64), Mpeketoni (94), Chuo cha Garissa (147), Mandera (zaidi ya mia) na mauaji ya kiholela kila mara kuanzia Mombasa, Nairobi, Garissa, Wajir, Lamu, Malindi na maeneo mengine mengi kote nchini.

Baadhi ya polisi wamegeuka na kuwa magaidi wanaowaua na kuwadhulumu Wakenya wasio na hatia badala ya kupambana na maadui wa taifa. Kila kukicha, Kenya ni vihoja. Kamanda anayetegemewa na wakenya ni Uhuru Kenyatta ambaye ni amiri jeshi mkuu wa majeshi yote. Kwa hivyo, rais anafaa kuacha kupiga siasa na kukabiliana na hali hii ya kuzorota kwa usalama.

Ufisadi

Serikali ya sasa bila shaka ndio fisadi zaidi tangu Kenya kujipatia uhuru. Jubilee imebaka demokrasia na kuiacha taifa nzima uchi wa mnyama. Hii ni serikali ambayo haiogopi kuiba. Wakenya wanazidi kuhofia utawala huu wa kiimla miaka miwili iliyosalia.

Uongozi wa serikali ya Jubilee ni ya kujipiga kifua huku wakijisifu kuwa wanatoa nafasi kwa vijana na badala yake kutoa nafasi kuzidi kuwahangaisha Wakenya na kuwatoa kwenye umaskini hadi kwenye lindi la ufukara.

Ahadi tasa

Kama kuna tuzo za hadithi za daganya toto jinga duniani hakika serikali yetu hii ingelishinda bila wapinzani. Ahadi tasa za tarakilishi, makazi kwa vijana, afya bora, viwanja kwa kila kaunti, usalama, huduma bora za afya miongoni mwa ahadi zingine butu zinazozidi kutolewa.

Sheria za jangwani

Serikali ya Jubilee imelemaza kila kitu. Haiheshimu sheria iliyowaweka mamlakani. Haiheshimu hata Mungu, kwani kwao kucheza na jina la Mungu ni sawia na mchezo wa kamari. Hii bila shaka ndio serikali inayoongoza kwa maombi ya kutafuta sifa kama wafarisayo tangu enzi za watangulizi wao.

Wakiomba ni lazima tujue, wakitoa sadaka lazima wadhibitishe kwetu kwa kupiga picha wanavyowasaidia wananchi ambao wao hao ndio waliowafanya maskini. Wanaombea matumbo yao na shida walizozileta wao wenyewe.

Wamesahau kuwa watu zaidi ya elfu moja waliouawa kinyama mwaka wa 2007/08 pia walikuwa na Mungu, walikuwa na familia, walikuwa na shida kama wao, walikuwa na watoto, walikuwa na marafiki kama wao, walikuwa na majirani kama wao. Tofauti kati yao ilikuwa ni pesa na dhulma za nguvu za uongozi wao uliowaletea shida chungu nzima.

Nashukuru Mungu maombi yao yanajibiwa. Kila ndimi inajitoa na kutaja njama zilizopangwa, njama zilizosababisha mauaji ya makumi ya watu. Mungu wanayemchezea atawajibu kupitia maombi hayo hayo ya kinafiki.

Ukabila

Hamna wakabila kama viongozi wa serikali hii. Wamegeuza Kenya na kuifanya soko huru la ukabila. Hawana soni wala hawaogopi Mungu. Vyeo vyatolewa kikabila kwa lengo la kukinga uongozi wao. Wanasahau kuwa kabila halitawasaidia kwani kila wanapofanya dhulma, hata makabila yao yanaumia. Kila wanapoongeza bei ya vyakula hata kabila lao linanunua kwa bei hiyo hiyo.

Mauaji ya kiholela

Ni nani anayewaua Wakenya? Ni nani aliyemuua mbunge wa kabete? Ni nani aliowaua viongozi wote wa kidini Mombasa? Ni nani aliye na nguvu ya kuua na kuzika vijana huko Wajir? Ni nani anayewateka nyara vijana mjini Nairobi, Mombasa, Malindi, Lamu, Garissa, Mandera na Wajir?

Ni nani anayewapiga risasi vijana kote nchini kwa madai ya uhalifu? Ni nani aliyewaua vijana wawili wa chuo kikuu cha Egerton? Iwapo serikali haina jawabu basi hatuna budi kusema kuwa serikali ndio inayowaua Wakenya na kuwapora kwa jina la usalama kwa wote.

Sijaona serikali inayowapoteza vijana wake huku ikijifanya ni serikali ya vijana. Kati ya haya yote niliyoyazungumzia, kinachoniudhi sana ni serikali isiyojali uhai wa binadamu.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Wasiliana naye kupitia [email protected]; [email protected]; FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali ama Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Similar Articles

.

Recommended Articles