Wanaume kazini [Picha: Hisani]

Mchwa ni mmojawapo ya wanyama ambao ni wadogo saana lakini ni mnyama ambaye anasifa kedekede kutokana na kazi yake.

Japo mchwa hafanyi kazi pekee yake, bidii yao wakiwa kwenye vikundi ndio funzo kwetu.

Ndiposa wakati huu ambapo mwaka mpya bado ni mbichi nikaona ni kheri tujikumbushe kuhusu mmojawapo ya nguzo muhimu katika kuafikia makuu maishani — yaani kufanya kazi kwa bidii.

Najua ni swala ambalo tulianza kulisikia tukiwa bado watoto au hata vijana barobaro. Naam, umuhimu wa kutia bidii kwa lolote tufanyalo maishani. Na kuwa hatima ya kufanya hivyo ni mavuno yenye kuridhisha.

Bila shaka wanafunzi ambao walifanya mitihani yao ya KCPE na KCSE mwaka wa 2016 watanielewa vyema nizungumziapo swala hili

Kumbuka kwamba hakuna chochote ambacho utaweza kuafikia maishani bila bidii — nimewaona watu wengi mno wakichukulia mzaha swala la kazi wanazofanya kila siku. Unapata kuwa jamaa ameajiriwa kazi, lakini unapata mienendo yake ya kazi ni ya kusikitisha sana.

Hana msukumo wowote wa kufanya kazi — hawa ni wale watu utawasikia wakisema kuwa “bora nionekane kazini na bosi wangu kwisha mshahara nitaukuta kwenye benki”

Watu kama hawa hawajali, mradi wapate mshahara. Hawana msukumo wowote wa kufanya kazi ila tu kwa kuwa watapata fedha.

hatima yao hata hivyo, huwa sio mwema. Kumbuka kuwa ukipanda mahindi usitarajie kuvuna maharagwe baada ya msimu wa kuvuna ukiwadia. Mwaka huu mpya tuna nafasi murwa ya kuanza upya. Iwapo mwaka uliyopita ulikosa msukumo na bidii basi mwaka huu tia bidii — amka asubuhi na nia mpya ya kuwa na bidii kama ya mchwa.

Amka kila asubuhi na wazo la kuwa unataka kazi yako ijitokeze mbele ya watu — yaani unataka bidii ya mikono yako itambulike, na haijalishi uko katika kitengo kipi ofisini. Kama wewe ni jamaa wa kufagia, jameni fagia kwa bidii ya mchwa.

Kama wewe ni mpishi pika chakula kwa bidii na ujue kuwa baada ya muda bidii hiyo itakusimamisha mbele ya wafalme.

Mungu aliumba dunia kwa bidii, hivyo yeye pia anatazamia kuwa tuwe watu wa bidii.
Cha pili, jameni mwaka huu mpya tusiwe watu wa kunung’unika kila wakati. Unapata kuna watu ambao hawaridhiki na chochote ni watu ambao hawatosheki — wanapata lawama katika kila kitu wanachofanya.

Hivyo basi inakuwa vigumu kufanya kazi nawao — jameni maishani wakati mmoja mambo huenda yakawa na kasoro moja au nyingine.

Bora tusiwe watu wa minong’ono ya kila aina kila kuchao — leo ni hiki, kesho ni kile. Jaribu kufanya uwezalo kupitia ulichonacho na hatimaye mambo yatakuwa shwari.

Siku hizi vijana wanaamini kuwa wanaweza kuwa tajiri katika kipindi kifupi mno — eti haijalishi unachofanya bora waweza endesha gari kubwa.

Unanyumba ya kistarehe na unavalia nguo za kisasa basi umeshafika! Jameni usidanganyike, ili uwe na utajiri wa kudumu lazima kazi utafanya kwa bidii.

 Utajiri unaopatikana kwa siku mmoja vivyo hivyo ndivyo upoteavyo. Tuwe watulkivu na wenye bidii maishani. Nakutakia mwaka mpya ambao utakuwa na bidii ya mchwa baraka !

Wasiliana nami [email protected]