Raia wa Venezuela kuhojiwa kwa mara ya pili na DCI

Raia 3 wa Venezuela waliokamatwa wakisafirisha vibandiko vya kutumika katika uchaguzi mkuu, Jumatau watahojiwa kwa mara ya pili katika Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi, DCI.

Washukiwa walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA, wakisafirisha vibandiko hivyo vilivyokuwa na nembo za Tume ya Uchaguzi, IEBC.

Jose Comargo Gregorio, Joel Gustavo Rodriguez Garcia na Salvador Javier Sosa Suarez walimatakwa Alhamisi iliyopita na kuhojiwa kisha vifaa hivyo kuchukuliwa na polisi.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alikashifu kukamatwa kwao akisema hatua hiyo ingetatiza shughuli za maandalizi ya uchaguzi.

Haya yanajiri huku Chebukati akitarajiwa kutoa taarifa kamili kuhusu kunaswa huko wakati cheche kali zinaendelea baina ya mirengo ya Azimio na Kenya Kwanza kuhusu suala hilo.

Azimio inataka maelezo zaidi kutoka kwa IEBC, Kenya Kwanza ikisema shughuli za tume hiyo hazifai kuingiliwa.