×
App Icon
The Standard e-Paper
Kenya’s Boldest Voice
★★★★ - on Play Store
Download App

Wakenya watahadharishwa kuhusu jua na ukame

 

Wakaazi wa Bungale, Magarini, kaunti ya Kilifi wajaribu kuoko mifugo wao kutokana na miale ya jua kali. [File, Standard]

Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga imewaonya Wakenya kujiandaa kwa kipindi cha jua kali na ukame chenye joto ya juu ya wastani katika siku 28 zijazo.

Idara hiyo imesema kuwa sehemu kubwa ya nchi itashuhudia joto kali hadi mvua zitakapoanza mwezi Machi.


Kwa mujibu wa taarifa ya Idara hiyo, mvua za hapa na pale zinaweza kunyesha katika miji kama Nairobi, Mombasa, Kisumu, Kericho, Nakuru na Kiambu, lakini maeneo mengi yataendelea kuwa makavu na yenye joto zaidi kuliko kawaida.

Idara hiyo imewasihi wananchi kuchukua tahadhari, ikiwemo kunywa maji mengi na kujilinda dhidi ya magonjwa yanayohusiana na joto kali, hasa kwa watoto, wazee na watu wenye magonjwa sugu.

Wataalamu wa hali ya anga wanasema kuwa mwezi wa Machi huenda ukaashiria mwanzo wa msimu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi, huku mvua kubwa zaidi na zilizoenea zikitarajiwa mwezi Aprili.

Hali hii ya ukame inachangiwa na mifumo ya hali ya anga kama vile La Niña na Dipole hasi ya Bahari ya Hindi, maarufu kama negative Indian Ocean Dipole. Mifumo hiyo kwa kawaida husababisha hali ya hewa kavu zaidi katika eneo la Afrika Mashariki.

Kutokana na hali hiyo, Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini limehimizwa kuongeza vituo vya kunywea maji kwa wanyamapori ili kupunguza hatari ya moto wa misitu na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Vilevile, mamlaka za serikali na mashirika ya kibinadamu zimetakiwa kuchukua hatua za haraka, ikizingatiwa kuwa ukame unaweza kuzidisha uhaba wa chakula na kuathiri uzalishaji wa umeme wa maji.

Kwa upande wa halijoto, maeneo ya nyanda za chini na kame, hasa kaskazini-mashariki na kaskazini-magharibi mwa nchi, yanatarajiwa kushuhudia joto la mchana linalozidi nyuzi joto 30, huku baadhi ya maeneo yakifikia kati ya nyuzi 32 hadi 35.

Maeneo ya pwani na ukanda wa Ziwa Victoria, ikiwemo Kisumu, yanatarajiwa kuwa na halijoto ya mchana ya takriban nyuzi 31 hadi 33.

Hata hivyo, Nairobi na maeneo ya nyanda za juu yatabaki na hali ya hewa ya wastani, huku joto la mchana likitarajiwa kuwa kati ya nyuzi 26 hadi 27, na halijoto ya usiku kushuka hadi nyuzi 12 hadi 14.