Ukitaka kumuua sokwe usimwangalie usoni! Leo hii yanibidi kuwasemesha wanahabari wenzangu.
Nchi hii ya Kenya kila jambo ni kama laendeshwa na kuongozwa kwa misingi ya kikabila, hivi kwamba ukiliona tu jina la mtu basi wamhusisha na kabila fulani, timu fulani au hata chama fulani cha siasa.
Lakini huo sio ukweli wa mambo. Tusichukulie tu kuwa kila mzawa wa eneo la Nyanza ni mfuasi wa mrengo wa CORD au chama cha ODM ama ati mwafulani kwa kuwa kazaliwa eneo la Kati ya nchi basi ni mfuasi sugu wa mrengo wa Jubilee Party! Sivyo abadan katan!
Ingawa hivyo, leo hii Wakenya wanazifungulia idhaa za redio, vituo vya runinga na majarida au magazeti yachapishwayo nchini wakijua wazi ni habari gani watazisikiliza, kuzitazama au kuzisoma kwa kutegemea mmiliki wa chombo hicho husika cha habari.
Upo uwezekano kuwa sera za vyombo vya habari nchini, tukirejelea uhariri na ni habari zipi zitapewa kipaumbele vinatagemea pakubwa wamiliki wa vyombo hivi vya habari na pia wahariri wahusika ambao huwasukuma maripota na wapiga picha kupiga picha kwa kutegemea mrengo upi wa siasa. Kenya inajiandaa kwa zoezi la uchaguzi mkuu mwakani. Wanasiasa na vyama vyao wameanza mapema mikakati ya ‘kuwanasa’ na kuwapa chambo maripota, wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari. Kwa hakika hili si jambo jema. Vyombo vya habari vinatawaliwa na madai ya hongo. Mara nyingi watasema tangazo hili ni la mteja, makala haya yamelipiwa na chama au mwanasiasa fulani kumbe sivyo.
Kama ni makala yaliyolipiwa shilingi laki mbili, na hapo pia hongo kupenyeza vitanga, basi makala na taarifa za nusu saa, vitaongezwa robo saa ya “bwerere”. Picha hii ilijitokeza bayana majuzi kwa namna idhaa zetu zilivyopeperusha na kisha magazeti yetu kuandika kuhusu sherehe za kuundwa kwa chama kipya cha Jubilee Party, sherehe za miaka kumi ya ODM. Na kisha kampeni za jiji la Nairobi zilizofanywa na Jubilee Party na ODM jijini Nairobi. Twaelekea wapi jamani wanahabari? Leo nimesema. Sitokubali kamwe kutapikia nyongo yangu kaburini. Mola wangu anilinde.
Hassan Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha @radiomaisha [email protected], [email protected], FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali, Twitter: @alikauleni
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media
platforms spanning newspaper print
operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The
Standard Group is recognized as a
leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national
and international interest.