×
App Icon
The Standard e-Paper
Home To Bold Columnists
★★★★ - on Play Store
Download Now
×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Jicho Pevu: Je, nani atasema Raila tosha 2017

Living
 Cord leader Raila Odinga

Kenya ya sasa isingekuwa Kenya bila juhudi za baadhi ya wananchi walioona umuhimu wa kupiga vita ukoloni mambo leo, ujakazi, ukosefu wa elimu na mengine mengi.

Hivyo ni aibu kubwa pale mtu aliyeteswa gerezani, mtu aliyepigania mabadiliko ya katiba na hata kuiweka ukabila pembeni na kusema “kibaki tosha’’ anapodhalilishwa na kuonekana kama asiyekuwa na umuhimu kwa taifa hili.

Ni wazi kwamba historia ya Kenya haiwezi kuandikwa sahihi bila mchango wa Raila Odinga. Iwapo kuna funzo kuhusu uzalendo na kutupilia mbali maslahi basi aliyekuwa rais Mwai Kibaki ana ushuhuda wa kutosha juu ya suala hilo kwani kama si Raila Odinga asingekuwa rais. Je Agwambo alimpa Kibaki usukani mwaka wa 2002 akiwa mluo mwenzake?

Aliwaonyesha njia wengi

Ni Raila aliyewaonyesha njia wengi miongoni mwao naibu wa rais William Ruto, lakini malipo yake yamekuwa maamuzi ya wakenya kubadilishwa kwa lengo la kumnyima nafasi ya kwenda ikulu.

Baada ya uchaguzi wa 2007, alikubali serikali ya muungano kwa faida ya kumwezesha mkenya kujikwamua katika lindi la umaskini wa pesa na wa fikra.

Mnamo mwaka wa 2013, punde tu baada ya uchaguzi, Raila alielekea mahakamani kutafuta haki.

Aliiweka utaifa mbele na kukubali maamuzi ya mahakama. Je, Raila alilaani taifa hili? Je Mungu analipa taifa hili kwa maovu aliyotendewa? Ukitafakari majibu ya maswali haya nakukumbusha kauli alizotuachia; “Democracy is on trial’’.

Kauli ambayo imekuwa sawa na saratani ikitumaliza siku baada ya siku. Bunge limekuwa soko badala ya uwanja wa sheria sasa wananadi sheria kwa misingi ya kuiridhisha serikali ya Jubilee.

Mumemwona Adan Duale?

Mwaka 2017 bila shaka tutaona mabadiliko kwani nchi hii si ya ‘mama yao wala baba yao’ — asemavyo Adan Duale.

Duale, kiongozi wa wengi bungeni leo anakula kiapo kwamba yupo tayari kupigwa risasi ili kumwokoa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto.

Swali ni, Mbona huyu kiongozi aliyeletwa bungeni na watu wa Garisa asianze kuwaokoa wanananchi wanaopigwa risasi na kuuawa ovyo katika kaunti yake na kaunti jirani za Wajir na Mandera?

Kila kipindi cha sala washika udhu na baada ya sala watetea udhalimu. Wajifanya hamnazo kucheza ngoma, utakapojiuliza mbona umepewa jukumu la kubweka kila mara ilihali maendeleo katika eneo lako hamna. Kama ulishindwa kutoa orodha ya wanaofadhili ugaidi kama ulivyoahidi, basi orodha tunayo ya watakaokuangusha debeni 2017.

Mumekuwa limbukeni wa mitandao lakini kumbukeni kila anayejichamba na matawi ya mgomba daima hubakia na kinyesi chake.

Kumbukumbu

Nikirudia swala langu, ni wazi kuwa uongozi wa jubilee unafanya biashara na maisha ya wakulima wa miwa na wafugaji ili kupata pesa za kampeni.

Mara nyengine nashindwa kulaumu viongozi hawa kwani mtu asiyejua aendako hawezi kupotea njia.

Kumbukumbu zangu zanipa taswira ya mabango yake Rais wetu mara ya kwanza alipojitosa katika ulingo wa kisiasa ‘UHURU NA KAZI” kisha baadaye muungano wa ‘KUSEMA NA KUTENDA’ .

Je, haya manyanyaso, ubaguzi wa misingi ya kidini na mauaji yasio kifani yanaenda sambamba na kauli hizi?

Leo majangili wamefanya nchi yetu uwanja wa mazoezi huku viongozi wetu wakitumia matukio haya ya kinyama kuonyesha ubabe wao na baadhi wakiuza sura.

Anachosahau Rais ni kwamba hata upige mbwa vipi kama nyumba inanukia nyama mbwa atarudi.

Nani atasema Raila tosha?

Kilichotokea mwaka 2002 pale makabila na vyama vyote vilikuja pamoja na kumkataa rais na chaguo lake wakati huo Uhuru Kenyatta, ndivyo vitakavyoandikisha historia upya kwa kuing’oa serikali ya Jubilee.

Nimemwona Raila Odinga katika umri wangu na daima jezi yake imekuwa ya kunasua taifa hili. Raila hakuwa mwendawazimu aliposema ‘Kibaki Tosha’ licha ya kujua fika Mwai Kibaki ni mkikuyu na pili kujua alivyofanywa babake Jaramogi Oginga Odinga miaka ya nyuma. Je, hapakuwa na makabila mengine? Je, mkikuyu yupi yupo tayari kusema Raila tosha?

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Trending Now

.

Popular this week

.

Similar Articles

.

Recommended Articles