Asasi sufufu za kimataifa hususan za kifedha zimethibitisha kuwa Afrika ni sehemu pekee duniani ambayo ina raslimali za kiuchumi kushinda sehemu nyingine. “Simba wa Afrika anamwambia simba marara (Tiger) wa Asia kwamba nimekalia mali na nakuja kutawala,” asema kimafumbo Raila Odinga katika hotuba yake ya umoja wa wafanyikazi Afrika jijini Nairobi majuzi. Raila anamini kuwa Afrika ina uwezo wa kuwa mbele kimaendeleo kushinda mabara mengine kama Ulaya na Amerika. Swali ni, Je, kuwaje Afrika iliyo tajiri kuwa kama masikini anayeomba misaada kwa ‘matajiri’ wa nje?
Je, ni sababu zipi za kinaya hiki cha Afrika na suluhu iko wapi? Sambamba na imani ya Raila aliye mjumbe maalum wa miundo mbinu katika Umoja wa Afrika (AU) ni kweli Afrika imelalia masikio. Penye miti hakuna wajenzi. Msemo huu ndio ukweli uliopo kwa bara la Afrika na ni changamoto kubwa katika karne hii ya utandawazi inayotowa fursa ya kuendelea badala ya kuzembea.