Mwanadamu ameumbwa na kuwekwa katika mazingira ambayo inamlazimu kuugua au kuwa mgonjwa kutokana na sababu mbali mbali. Hata hivyo imebainika wazi kwamba wanawake huathirika zaidi na baadhi ya magonjwa kuliko wanaume. Mwanamke ana magonjwa maalum yanayomsibu kuliko mwanaume. Zaidi ya hayo magonjwa ya wanawake hayafanyiwi upekuzi wa mapema kulingana na wataalamu, na majaribio mengi ya madawa hayashirikishi masuala ya wanawake.
Kuna magonjwa kadha ambayo hayo yanawasibu mno wanawake yakiwa ni pamoja na saratani ya matiti, saratani ya mfuko wa uzazi, kufikia kukoma kwa siku zao za hedhi, na mimba. Wanawake hupata magonjwa ya mshtuko wa moyo na kuwasababishia vifo kuliko wanaume. Kupata dhiki za moyo na wasiwasi ni magonjwa ambayo humkumba zaidi mwanamke anapougua. Mbali na hayo mwanamke hukabiliwa zaidi na matatizo ya njia ya haja ndogo yaani mkojo, kuliko wanaume, na magonjwa ya zinaa pia huleta madhara makubwa kwa wanawake. Miongoni mwa magonjwa ambayo humsibu mwanamke zaidi magonjwa manane yanayofuata ndiyo yanayomvamia mara kwa mara zaidi na kutishia hali yake ya afya.