Eneo la Kisauni linaoongoza katika ukusanyaji wa saini 200, 000 zinazolenga kuvunja bunge la Kaunti ya Mombasa

Kufikia sasa Eneo Bunge la Kisauni ndilo linaoongoza kwenye shughuli ya ukusanyaji wa saini 200, 000 kwenye maeneo bunge yote sita ya Kaunti ya Mombasa zinazolenga kulifanikisha lengo la kulivunja bunge la Kaunti hiyo.

Takwimu ya Vuguvugu kwa jina Oparesheni Fagia Bunge ambalo linaendeleza shughuli hiyo zinaonesha kwamba kufikia sasa jumla ya saini 10, 537 zimekusanywa eneo la Kisauni, likifuatwa na Mvita ambako jumla ya saini 10, 081 zimekusanywa, kisha Likoni ambako saini 9, 452 zimekusanwa, Nyali saini 8, 193, Changamwe saini 8, 059 na hatimaye Jomvu saini 4, 636 zimekusanywa.

Shughuli hiyo inayoongozwa na makarani mia moja na wasaidizi watatu katika kila wadi ambao wanatumia mfumo wa sasa kutekeleza ukusanyaji huo iliyozinduliwa rasmi siku sita zilizopita.

Muda wa wiki nne uliwekwa kwa utalekezaji wa shughuli hiyo kabla ya saini hizo kuwasilishwa kwenye idara zinazohusika ili kuufanikisha mchakato wa kulivunja bunge hilo. Mgandi Kalinga ni Katibu wa Vuguvugu hilo.

Hatua hiyo inajiri kufuatia malalamiko ya baadhi ya wakazi wa Mombasa walioanzisha vuguvugu hilo kufuatia madai kwamba baadhi ya Wawakilishi wadi wamekuwa wakizembea kwenye majukumu yao.

Wakazi hao wanalalamikia pia hatua ya Wawakilishi wadi hao kuingilia utendakazi wa Wakuu wa Utawala kwenye Kaunti ndogo zote sita za Mombasa.

Jingine wanalolalamikia ni hatua ya kutaka kubanduliwa mamlakani kwa  mawaziri wa Uchukuzi Tawfiq Balala, Waziri wa Michezo Munyoki Kyalo na wa ardhi Edward Nyale.

Related Topics