Ripoti kamili kuhusu sakata ya kupotea kwa shilingi bilioni 5 kutolewa wiki ijayo

Na Carren Omae

''Ripoti kamili kuhusu matumizi ya fedha za wizara itatolewa wiki ijayo''. Kauli hiyo ni kulingana na Waziri wa Afya Cleopa Mailu. Akiwahutubia wanahabari ofisini Mwake kuhusu madai ya kupotea kwa shilingi bilioni tano katika Wizara hiyo, Mailu amesisitiza kwamba taarifa zinazoendelea kutolewa kuhusu sakata hiyo zinahusu ripoti ya uchunguzi ambayo haijakamilika.

Waziri huyo hata hivyo amesema kwa sasa hakuna afisa yeyote atakayeondoka ofisini kabla ya uchunguzi huo kukamilika, huku akisema iwapo madai hayo ni ya kweli waliohusika watachukuliwa hatua.

Hata hivyo Kinara wa Muungano wa CORD Raila Odinga ameshtumu taarifa kwamba uchunguzi wa sakata hiyo unaendelea. Kulingana na Raila Rais Uhuru Kenyatta ameshindwa kukabili tatizo la ufisadi.

Hayo yanajiri huku shinikizo zikiendelea kutolewa kwa Waziri Cleopa Mailu, Katibu Mkuu wake Nicholous Muragori na aliyekuwa Waziri wa afya ambaye sasa ni waziri wa Uchukuzi James Macharia Kujiuzulu. Seth Panyako ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Nchini.

Panyako amesema ufujaji wa fedha za umma ndio umesababisha matatizo ambayo yanaikumba sekta ya afya. Kulingana naye ni jambo la kusikitisha kwa wagonjwa kuendelea kuhangaika hasa wanaotafuta huduma katika hospitali za umma ilhali maafisa wakuu serikalini wanahusika katika ufujaji wa fedha zilizotengewa huduma za matibabu nchini.

?Ametishia kwamba huenda wauguzi kote nchini wakashiriki mgomo kushinikiza uchunguzi wa kina kufanywa kukabili tatizo hilo.