Je, ni kweli Karume alisaliti Wazanzibari kwa kuuza nchi?

Huku shamrashamra zikinoga kuadhimisha miaka 55 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar maswali mengi yanaulizwa na wadadisi kuhusu muungano huu. Je, muungano huu ulijijenga katika mazingira yapi? Nani waasisi wa muungano huu?

Je, wananchi wa pande zote mbili za bara na visiwani waliruhusu kisheria kuwa na uhusiano huu? Ukweli wa mambo ni kuwa muungano huu ulianzishwa na marafiki wawili wa jadi yaani Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika na Abeid Amani Karume wa Zanzibar. Wawili hawa walitia sahihi zao katika mkataba wa kuunganisha ardhi zao kuwa moja mnamo tarehe 22 Aprili 1964 kule Zanzibar ambapo Nyerere aliunganisha michanga ya bara na visiwani kuashiria umoja huu.

Hatahivyo, kisheria muungano haukukubalika kwani kanuni hazikufuatwa ama zilipuuzwa. Bunge la Tanganyika lilipitisha kwa haraka mkataba huu lakini bunge la Zanzibar lilipinga. Wakitumia udikteta Nyerere na Karume walipitisha mkataba na kuutekeleza.

Wengi haswa wazanzibar hawakupendezwa na hatua hii ya kiimla na mpaka sasa wazanzibar wengi wanaupinga. Makame Mtumwa Makame, mzee wa kipemba anayeishi kusini mwa Pwani ya Kenya, asema ilikuwa dhulma kwa wazanzibar kuporwa ardhi na haki yao na Nyerere kupitia kwa Karume. “Karume alitusaliti kwani hatukushauriwa kama wadau wa taifa,” alalamika Mzee Makame na kudai kuwa Zanzibar ilipoteza hadhi, uhuru na asili yake kubwa kuungana na Tanganyika bara.

Tukirudi nyuma ya msingi wa muungano huu inadhihiri kuwa Karume alitaka usaidizi ili ajijenge kisiasa dhidi ya wapinzani wake wa ndani na nje. Baada ya Uingereza kuondoka Zanzibar walikabidhi utawala wa nchi kwa watawala wa kale wa kiarabu wa asli ya Oman. Karume pamoja na vuguvugu la uhuru wa mtu mweusi waliushirikiana na Nyerere na kupanga njama za kupinduwa utawala wa kisultan. Karume alishauriana na Nyerere ambaye alipanga wapiganaji wa kukodisha walioongozwa na Field Marshall John Okello kutoka Uganda. Okello na wapiganaji hao walituwa Zanzibar na kuwauwa takriban watu elfu 20,000 wengi wakiwa waaarabu na washirika wao.

Yasemekana mashekhe wakubwa wa kiislamu waliuliwa na chinjachinja huyo muuwaji wa Uganda.Pia wanawake wengi walibakwa. Ni wakati huo ambapo wakimbizi wengi wa Zanzibar haswa Pemba walipohamia Kenya kwa wingi pamoja na familia zao. Mmoja wa wakimbizi hao ni  alikuwa kadhi mkuu wa Zanzibar na msomi mkuu wa kiislamu marehemu Sheikh Adbulla Saleh Farsy.Serikali ya Kenya ilikubali awe kadhi wa Kenya.

‘Ilikuwa sikitiko kwa familia kutengana na mateso kwa wengi’ asema Makame akiongeza kuwa Karume alifanya kosa kuruhusu mauaji hayo. Makame asema ingekuwa ni sawa kumpenduwa tu Sultan wa Zanzibar badala ya kuuwa watu bure na kumwaya umwagikaji mkubwa wa damu. Sultan wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah pamoja na familia yake waliokolewa na majeshi wa Uingereza na kusadirishwa Uingereza alipokaa hadi kifo chake huku nyuma washirika wake wakichinjwa kama kuku. Karume akiwa mwenyekiti wa baraza la mapinduzi alidhibiti utawala wake lakini wengi walimpinga kwa udikteta wake.

Jamaa ya maelfu walouliwa walizidi kumchukia na kupanga kulipiza kisasa. Okello alizidi kutakabari na hata  kudhani angepewa cheo kisiwani lakini naye baada ya kutumika aliamriwa na Karume aondoke Zanzibar. Ilkuwa mnamo mwaka 1972 wakati Karume alipouliwa katika mkutano na hapo wanachama wa upinzani wa chama cha Ummah Parti wapatao 40 walipotiwa nguvuni pamoja na kinara wao Abdurahman Mohammed Babu. Wasomi wengi wa Zanzibar walihama na kwenda Ulaya huku wakifanya mikakati ya kukombowa nchi yao toka kwa muungano wasoutaka na Tanganyika.

 Muungano huu ulibadili majina asili ya nchi hizi na kuzaa nchi ya Tanzania. Kimsingi Rais wa kwanza wa muungano ni Julius Nyerere huku makamu wa kwanza wa rais akawa Karume. Makamu wa pili wa Rais alikuwa Rashid Mfaume Kawawa toka bara. Aghalabu vyama viwili vya kisiasa vya nchi hizi vilivunjwa na kuzaa chama kimojacga TANU kabla ya kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wanaopinga muungano huu wanadai haukuleta faida yoyote bali madhara haswa kwa wazanzibar. Mwanafunzi wa kizanzibar wa chuo kikuu mchini Kenya Kibibi Ramadhani asema wa zanzibar bado wako katika ukoloni wa Tanzania.

 ‘Hatuna uhuru kila kitu kinaendeshwa bara na hadhi yetu pamoja na historia yetu imebomolewa na watanganyika’ alalamika Kibibi huku akiwalaumu Karume na Nyerere kwa kuzuwa masahibu hayo. Marehemu Abdurahmani Babu aliyefungwa na Nyerere alipinga sera za kiuchumi aloleta Nyerere za ujamaa na kujitegemea. Siasa za ujamaa na kujitegemea kupitia kwa azimio la Arusha pia liliathiri Zanzibar kwani ilibidi nao waishi katika mfumo huo tatanishi.

 Mzee Makame asema wazanzibar na watanganyika ni kama mbingu na ardhi kifikra, kiuchumi na kijamii.Asema huwezi kulinganisha mtu wa bara na kisiwani. Kwa muktadha huu Zanzibar ni visiwa vyenye raslimali kubwa na vitega uchumi hususan katika sekta ya utalii na kilimo. Zanzibar inaongoza duniani kwa kukuza kilimo cha karafuu. Mashamba makubwa ya  karafuu yalianzishwa na Sultan wa kwanza wa Zanzibar Seyyid Sayigd aloboresha pakubwa uchumi wa Zanzibar.

 Nyakati hizo Zanzibar ilikuwa kituo kikubwa cha uchumi katika kanda hii kwani Sultan alikuwa akimilki ardhi yote ya bara. Inaweza kukubalika kuwa kama Zanzibar haingeungana na Tanganyika basi uchumi wake ungeimarika kwa kiwango kikubwa kushinda ilivyo sasa. Ukitathmini visiwa vyengine katika bara Hindi vilivyo huru bila muungamo utapata ni vyenye ukuaji wa kasi wa uchumi.

Tumeangazia katika makaal ya ‘Ijue Dunia’ chumi za nchi za kisiwani kama Ushelisheli na Mauritious ambapo nghi hizi zinaongoza zengine katika Afrika katika ukuaji wa uchumi. Wadadisi wa uchumi wanaamini kuwa kama Zanzibar haikuungana na Tanganyika basi ingeimarika kiuchumi.Hii ni kuwa ingekuwa na wananchi wachache na raslimali kubwa kuliko sasa ikiwa na Tanganyika kubwa yenye changamoto zake. Kwa muktadha huu wengi wanamlaumu Karume kwa kufanya haraka ya kuunda muungano huu bila kuangalia athari za vizazi vijavyo.

Wazanzibar na haswa wapemba wanalaumu Tanzania bara kwa kuwadhalilisha na kuwalazimu kuwa katika chama cha mapinduzi. Imedhihiri wakati ya chaguzi kumekuwa na umwajikaji mkubwa wa damu na kila mara wazanzibar hukumbilia Kenya kupitia shimoni Kwale na kupiga kambi. Ni kwa mtazamo huu ndipo Makame asema hakuna cha kusherehekea maadhimisho ya nusu kane ya mapinduzi.Asema:- ‘Ni heri kuomboleza miaka 55 ya mateso ya muungano huu usio na maana.’