Siasa za kupimana nguvu baina ya mirengo ya Azimio na Kenya Kwanza zinatarajiwa kuchacha katika Bunge la kumi na tatu, kutokana tofauti ndogo kati ya wingi wa idadi ya wabunge kati yao.
Mrengo wa Azimio umeongeza idadi ya wabunge wake katika Bunge la Kitaifa baada ya kupata ushindi kwenye chaguzi tatu miongoni mwa nne za ubunge zilizofanyika Jumatatu.
Kisheria, miongoni mwa wabunge mia tatu na thelathini na saba kwa kujumuisha wawakilishi wa kike arubaini na saba wa kaunti ambao hukaa bungeni, Azimio ina jumla ya wabunge 165 huku Kenya Kwanza ikiwa na 160.
Hata hivyo, Azimio imepoteza wabunge wake takribani kumi na saba ambao wamehamia mrengo wa William Ruto katika Kenya Kwanza, wakiwamo saba wa chama cha UDM na wengine 10 ambao walikuwa wagombea huru.
Hali hiyo inatarajiwa kuleta ushindani mkali wakati wa vikao vya kumchagua spika wa bunge, ambapo Kenya Kwanza imempendekeza Moses Wetangula na Azimio ikimteua Kalonzo Musyoka.
Katika Baraza la Magavana, mrengo wa Azimio umefikisha jumla ya magavana 26, huku Kenya Kwanza ikiwa na 21, akiwamo Kawira Mwangaza wa Meru ambaye alihamia upande wa Kenya Kwanza kutoka Azimio baada ya uchaguzi mkuu.