Na Hassan Ali Ndio maisha ati! Kila nafsi itayaonja mauti. Ni kauli yenye ukweli na isiyo pingamizi. Wakenya, na hasa tasnia ya habari, twaomboleza. Kifo kimetupoka mwanahabari mashuhuri na mtangazaji mwenye mbinu ya kipekee kwenye simulizi zake za YALIYOTENDEKA idhaa ya Radio Citizen. Mwanahabari jasiri-jagina: Waweru Mburu ametangulia mbele za haki. Nasi tu njiani pia. Letu ni kujiandaa. Mengi yamesemwa mno kumhusu Waweru Mburu. Nami niseme japo kiduchu. Waweru Mburu alikuwa kwenye jopo na Bw. Fred Afune lililonihoji na mwenzangu Willy Tuva. Tukaajiriwa Radio Citizen. Naikumbuka siku hiyo ni kama jana tu jamani. Nikafanya naye kazi akiwa bosi wangu: Mkuu wa idhaa ya Radio Citizen. Kazi yangu ya kwanza, niliajiriwa kwa mkataba. Nayakumbuka vema maneno ya Waweru Mburu: “Ali najua mshahara utakaonza nao si mkubwa. Lakini jikaze tu. Tutaangalia mambo.” Zilikuwa shilingi alfu kumi na tatu. Haikupita miezi mitatu, Waweru Mburu akaniita afisini na kunipa barua ya ajira ya kudumu. Akaniambia kuwa sasa najiunga nao KABISA ili niache kuandaa makala na vipindi nilivyoandaa Redio China Kimataifa, kwa kuwa vilikuwa vikipeperushwa idhaa ya taifa ya KBC, na wakati huo ilikuwa mshindani wa Radio Citizen. Katika kipindi changu cha lugha, BAHARI YA LUGHA, (nilikoshirikiana na Jilani wa Mbura), Waweru Mburu alinisadia kwa hali na mali. Akinipigia simu kuniuliza hili na lile, nami nikimuuliza hiki na kile kukihusu Kiswahili. Kumbuka alikuwa mwalimu wa Kiswahili. Mmoja wa walimu niliokuwa nikishiriki nao kipindi hicho alipoaga dunia, ndugu Eliud Murono (Mola amrehemu) Waweru Mburu alinifaa sana. Aliniliwaza. Na kisha kunituma kwa meneja wa fedha Bw. Bashiri. Mama Gathoni Macharia alikuwa kasafiri. Hivyo akakosenakana. Na ilitakiwa atie saini ndio nipewe hela za kusafiri na za kuwapoza wafiwa. Waweru Mburu aliiingilia kati. Nikapewa hela. Nikasafiri na kuifariji jamaa ya mwenda zake Murono huko Mumias. Mburu waniliza jamani. Naikumbuka siku hiyo ni kama jana tu jamani! Kipindi kigumu sana cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Tulilala na kukesha na Mburu studioni. Tulihubiri amani jamani. Hali ilikuwa mbaya! Mbona nakuona tu ukitupa nguvu na kutuhimiza kuhubiri amani redioni. Wakati mmoja tukitoka Road Show ya redio Citizen magharibi ya nchi. Usiku wa manane, tukasimamishwa njiani na maafisa wa polisi. Tulipojitambulisha kuwa ni watangazaji wa redio Citizen, wakauliza yu wepi Waweru Mburu. Walifurahi kukiona kiwiliwili cha YALIYOTENDEKA. Wakasema hivi: “Unatulima sana makala yako, punguza kidogo.” Tulicheka tukavunjika mbavu! Wiki hiyo Waweru Mburu alikuwa kawasuta maafisa wa polisi wa trafiki wanaopokea hongo. Ukiingia mkutano wa Waweru Mburu kisha uone kukiletwa pizza, jua tu mapema kuwa mkutano huo utachukua mchana kutwa! Alikuwa mzungumzaji si haba! Mara ya mwisho nimesema na marehemu nikimpongeza kwa makala ya YALIYOTENDEKA kuhusu uchaguzi wa soka nchini. Alivyowakemea wanahabari wafisadi walivyohongwa na wagombeaji wa FKF! Kifo jamani. Kimetupoka mtu wa watu. Nikuage ndugu yetu marehemu Waweru Mburu kwa ubeti wa mshairi na mwandishi mahiri Mohammed Ghassani: “Basi ukome pumzi, ghururini kunishika Nikashindwa kumaizi, kwamba kuna kuondoka Siku isiyo ajizi, wala isiyo na shaka Mke awe kizuka, wanangu wawe yatima.”
Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA). [email protected], [email protected], FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali, Twitter: @alikauleni
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media
platforms spanning newspaper print
operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The
Standard Group is recognized as a
leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national
and international interest.