Na, Sophia Chinyezi
Mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Narok Kaskazini, William Ole Ntimama yataendelea kama ilivyopangwa. Haya yanajiri baada ya Jaji wa Mahakama Kuu, Joseph Onguti kukataa kutoa agizo la kuyasitisha mazishi hayo kufuatia ombi lililowasilishwa na mwanamume anayedai kuwa mwana wa Ntimama.
George Njoroge Kariuki mwenye umri wa miaka arubaini na sita alifika mahakamani kutaka mazishi ya Ntimama yaliyopangwa kufanyika Jumatano, yaahirishwe. Kariuki anadai kuwa alizaliwa mwaka 1969 na kwamba Ntimama alimtelekeza na mamaye ambaye alimlea peke yake.
Hayo yakijiri, serikali imetangaza kwamba misa ya wafu kwa Ntimama itafanyika Jumanne wiki ijayo katika kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi. Akizungumza na wanahabari, Msemaji wa Serikali Eric Kiraithe amesema mwili wa Ntimama utasafirishwa kutoka Hifadhi ya Maiti ya Lee hadi Narok siku ya Jumatano ambapo atazikwa.
Kiraithe ametoa hakikisho kwamba usalama utaimarishwa na msongamano wa magari kushughulikiwa wakati wa hafla hiyo huku wajumbe wa kitaifa na kimataifa wakitarajiwa kuhudhuria. Ntimama alifariki dunia akiwa amelala nyumbani kwake eneo la Narok, Septemba 2 akiwa na umri wa miaka 86.
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media
platforms spanning newspaper print
operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The
Standard Group is recognized as a
leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national
and international interest.