×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Jicho pevu: Fazul, ulitumiwa kutudhulumu

Living
Mohammed Ali
 Fazul Mohammed, mkrugenzi mkuu wa baraza linalo ratibu mashirika yasiyo ya kiserikali Picha: The Standard

Mwanahabari yuapaswa kuwa na uhuru wa kutaga kama kanga, sio uhuru wa kutagishwa kama kuku. Yamkini kelele za inzi hazimzuii fisi kufaidi mzoga na ndio maana nimekuwa mstari wa mbele pasi kujali vitisho, inda na kejeli nikijua wazi kwamba inzi kufa kidondani ni haki yake ilhali raha ya nyuki iko asalini.

Leo nazungumzia Fazul Mohammed, bingwa aliyeingia ugaani kutaka kurusha ngumi za kitoto pasi na kufahamu kuwa wanamisumbwi hodari walikuwa wakimwangalia na jicho la tatu.

Fazul Mohammed, mkrugenzi mkuu wa baraza linalo ratibu mashirika yasiyo ya kiserikali, alionekana kama chaguo bora wa kupasisha propaganda za serikali na kutumiwa kupenyeza ndani ya waumini wa dini ya Kiislamu kutumia jina lake, ilimradi wakifurushana raia, wakae kando na kusema ni masuala ya Waisilamu kwa Waisilamu.

Fazul alijiona mkali kama simba na kusahau ule msemo wa simba hata awe mkali vipi, mimba ni lazima atapata tu! Jina lake lilianza kugonga vichwa vya habari kila kukicha. Sasa kitumbua kimeingia mchanga na wale wote wanaojifanya chapa kazi ndani ya serikali hii isiyojali haki ya msingi ya Wakenya, sasa wameanza kuona mwangaza. Hata aliyekuwa Rais Mwai Kibaki ameona hila ya serikali hii isiyoogopa hata Mungu.

Hii serikali imejaa matapeli wanaojifanya wokovu na weupe kama pamba mbele ya macho ya Wakenya. Saa imekuwa ni serikali ya kusema na kupora. Ni serikali inayotumia watu kama Fazul, jamaa aliyejipiga kifua na kujifanya kamanda baada ya kupewa nyadhifa za kuwahadaa na kuwadhulumu Wakenya chapa kazi.

Fazul alitumiwa kuwasumbua baadhi ya watetezi wa haki za binadamu nchini kwa kutoa lalama tasa dhidi zao. Fazul alifutilia mbali mashirika haya yasisyo ya kiserikali na kuyakosoa vikali kwa kutofuata kanuni za usajili huku mashirika kama Muhuri na Haki Afrika yakihusishwa na ugaidi.

Sasa zamu ya Fazul imefika, zamu ya yeye pia kufutwa kutoka nyadhifa zake kwani, ikiwe kweli chuo kikuu cha Egerton hakimtambui kwa kukosa kumaliza elimu yake na hivyo basi kutokuwa na shahada kutoka chuo hicho.

Fazul amepuzilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa alimaliza elimu yake na kutunikiwa shahada ya degree ya Biochemistry. Hata hivyo, polisi wameanza kuchunguza madai haya ili kujua ukweli wa mambo.

Itakuwa ni jambo la aibu na ulaghai wa hali ya juu Fazul akipatikana na hatia. Wakenya tayari wamechoshwa na matapeli wa ufisadi, waongo wakubwa, wabakaji wa demokrasia na wanafiki nambari moja serikalini.

Fazul, uko wapi sasa? Hebu tujibu kwa makini kuhusu swala hili la shahada yako. Fazul,  nakupa wosia kama ndugu na mdogo wako; fanya kazi lakini usitumiwe kudhulumu watu bila ya wao kufanya makosa. Leo hii unalaaniwa kila kona. Mombasa hupendeki, Garissa hata hawataki kusikia jina lako, Nairobi hata usiseme, hupendeki tena ndugu yangu.

Licha ya kutopendeka, kuna msemo unaosema mtoto akinyea paja halikatwi. Leo umepewa fursa, hatutalikata guu lako ila tutalipangusa kinyesi hicho na kuendelea kukupenda walakin, omba msamaha, sio kwa vyombo vya habari, ila waendee uliowadhulumu wakiwemo marafiki zako, faraghani na uwaombe msamaha.

Uliowaita walaghai sasa wameachwa huru baada ya mahakama kubaini kuwa hawana doa lolote. Nazungumzia Haki Afrika. Kama huna habari, nakupa sasa. Pesa zao zimeachiliwa, wote uliotaka wakose kazi sasa wamerudi kazini licha ya kuwahangaisha, sio wao kama wafanyakazi pekee, bali pia hata familia zao ziliokuwa zikiwategemea.

Hussein Khalid wa Haki Afrika alifanya kikao na Rais wa Marekani Barack Obama licha ya serikali kumuhusisha na tuhuma za kufadhili ugaidi. Hussein bado anafanya ziara huko Marekani na Ulaya na viranja wa dunia ambao wanamwona kama rafiki na mtetezi wa haki za binadamu.

Kama kuna magaidi Kenya, basi baadhi yao wamo ndani ya serikali hii ya kutusambaratisha. Nahitimisha kwa kusema haki hushinda kila mara hata kama itachukua muda. Kenya itasimama imara nasi pia hatutasimama maovu yakitawala.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Wasiliana naye kupitia [email protected]; FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali; Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Similar Articles

.

Recommended Articles