Je, Jomo Kenyatta aliacha mbegu Taita?

Charles Mlekenyi.

Inaweza kuwa wakati rais wa kwanza wa Kenya hayati Jomo Kenyatta alitaga mbegu katika maficho yake ya kati ya mwaka wa 1948 hadi 1952? Twajua hatujui lakini mara nyingi washwahili hunena; “Dalili ya Mvua mara nyingi huwa ni mawingu”.

Jomo Kenyatta alipowasili mafichoni kuishi ndani ya mapango ya Kino katika kijiji cha Mwanguwi kujumuika na mashujaa wenzake wa uhuru waliokuwa wamefichwa awali na mwenyeji wao shujaa Zephania Nyambu Mwakio taita ya Wundanyi, alijua wazi kuwa mikakati ya kuikomboa nchi nzima inahitaji mbinu mbadala.

Wanakijiji katika eneo hili mpaka vile jirani na Taita nzima kwa jumla, wanahisi kwamba msimamizi wa mapango haya leo hii huenda akawa ni mtoto wa Jomo Kenyatta kuambatana na kanuni za kitamaduni wa wema wa jamii hii hapo zamani.

Kulingana na mwanachama wa chama cha Wazee wa Njavungo, Ronald Mwasi na ambaye alikuwa mtu wa kwanza kumtambulisha mama Shujaa Silvia Manga Mwakio kwa rais Uhuru Kenyatta mnamo mwaka 2013 kama mlezi wa baba wa kwanza wa taifa miaka ya 1948-1952 kama mwenye kumshughulikia matakwa yake ya kila siku, mila na desturi iliruhusu jamii kuwepo uwezekano wa kumfadhili rafiki wakati shida ya kimahitaji ya kimwili endapo unao uwezo wa kuwa na mke zaidi ya mmoja.

Mwenyeji na shujaa Zephania Nyambu ambaye ndiye aliyekuwa mwenyeji katika mapango haya, alikuwa na wake wanne, Silvia Manga, mamake Charles Mlekenyi akiwa bibi wa pili. Kati ya wake wote hao, yaaminika huyu ndiye aliyekuwa kipusa aliyewapeleka mbia mashujaa waliokuwa wakijibanda mapangoni humo. Yaaminika leo hii, endapo kunaweza kujitokeza kwa mdhamini na kutaka kuwafanyia uchunguzi wa DNA, wazee wote walioko rika moja na Charles Mlekenyi, walio hai leo, watu watapigwa na butwaa kwani huenda kukapatikana damu na vizaliwa wa magwiji wengi kisiasa nchini.

MTOTO SI MTOTO

Leo hii, Charles Mlekenyi ambaye alizaliwa muda mfupi baadaye baada ya hali ya hatari nchini (State of Emegerncy) kutangazwa mnamo mwaka 1952, wengi wa wana vijiji na wadadisi chungu nzima wanasema kuwa huenda akawa alizaliwa kupitia kwa ushirikiano wa karibu wa kimaisha baina ya Mama shujaa Silvia Manga na Jomo Kenyatta kabla ya kusukumwa korokoroni kule Kapenguria akiwa na wenzake.

“Yashangaza kila jioni, majirani huenda wakachapa mtindi wao na hatimaye kunipitia hapa nyumbani kwangu kunikejeli kuwa utakuwaje maskini wewe mtoto wa hemaya ya kifalme ya Jomo Kenyatta ambapo wenzako wanayo mamilioni ya pesa na mifugo ya kutosha ilhali wewe wala ‘kimanga’ na kuchuchuta ng’ombe moja hapa” azungumza Charles Mlekenyi.

Je, wewe yaweza kuwa ulizaliwa na Mzee Jomo? Nilimuuliza.

“Watu wanasema hivyo lakini mimi sijui kwa kuwa wakati mtoto unapozaliwa huwa huna mkataba na mama yako ama babako kwamba nitazaliwa hivi ama vile. Mengi yanazungumzwa lakini kusema ukweli siwezi kukujibu swali lako na wala sijafanyiwa DNA kuthibitisha uwazi huo”, alinijibu Charles Mlekenyi.

Anasema kwa ufahamu wake, babake Zephania alimwelezea mengi kuhusu harakati zao za kutafuta uhuru wa Kenya wakati walipokuwa Taita pamoja. Vile vile mamake ambaye ameishi naye kwa miaka mingi hadi kifo chake mwaka 2015 hali kadhalika pia alimwelezea mengi kuhusu Jomo Kenyatta lakini kwa sababu za mila na ustaarabu wa kijamii, kamwe hawezi kumwaga mtama peupe.

“Ile naweza kukuambia ni kuwa Mzee wangu Zephania, Jomo Kenyatta na Mbiu Koinange walikuwa na muma wa karibu mno (uhusiano) na urafiki wa dhati. Kunao wakati ambao mama alinambia Mbiu Koinange alitutembelea na kumwuliza mzee kumtaja mtoto wake jina lake”, aongeza huku akisema kwamba kitinda mimba wao ambaye anaelekea umri wa miaka zaidi ya 50, alibatizwa jina la Mbiu Koinange Mwakio.

Charles Mlekenyi na mzee Ronald Mwasi wakiwa katika pango la Communist wakionyesha mahala Jomo Kenyatta alikua akiendesha mikutnao na Nyerere.

UKAPERA WA MUDA

Kulingana na Charles Mlekenyi Mwakio mwenye umri wa miaka sabwini na ambaye ndiyo anayamudu mapango haya, anaelezea kinaga ubaga juu ya kuwasili kwake Jomo Kenyatta na jinsi alivyokaribishwa kwa wema wote na babake Zephania. Mzee Zephania aliaga dunia ambaye kulingana na kumbukumbu ya kaburi lake alizaliwa mnamo mwaka 1906, aliaga dunia mnamo mwaka 1993.

Shujaa Silvia Manga, mamake Mlekenyi ambaye kwa Mzee Zephania ni mke wa pili kati ya vipusa wanne aliobarikiwa kuwaoa miaka hiyo ya nyuma, alifariki juzi mwaka wa 2015 akiwa na umri wa miaka 104. Ushujaa wake hatahivyo ulitambuliwa punde Rais Uhuru Kenyatta alipochaguliwa kuwa rais wa nne wa Kenya mnamo 2013 alipopata fursa ya kukutanishwa ana kwa ana na Wazee wa baraza la Wataita na Wataveta la Njavungo alipozuru kaunti ya Taita Taveta.

Akiwa kipusa wa makamu wakati huo, Shujaa mwendazake Silvia Manga ambaye hadi kufa kwake urembo kwake ulibakia ukithibitishwa na michoro ya kale kwenye sura, Jomo Kenyatta alimpendekeza na kumwia radhi mwenyeji wake Zephania, kumruhusu Silvia amhudumia kwa kila jambo ikiwa ni pamoja na kumwandalia chakula, kumfulia nguo na kumpeperushia umbu wanaosukumwa kwa upepo mkali na baridi nzito ya milima ya Taita.

MABOBESHI YA UINGEREZA

Kulingana maelezo ambayo yanathibitishwa na baadhi ya vifaa ambavyo aliacha nyuma kama vile kichana cha mkono cha kuchania nywele mtindo wake wa kusukuma nywele nyuma na cherehani cha kushonea nguo. Kwa kuwa alikuwa ni mlami mbele ya mashujaa wenzake, alijibobeshi vikali na kuwashinda wengine katika kubwagiza masharti ya jinsi atakavyoishi.

Mabobeshi yake, bila shaka yaliwavutia kina mama ambao walikuwa wakiwahudumia mashujaa hao akiwemo Pinto Gama Pinto, Jaramogi Oginga, Tom Mboya, Paul Ngei, Masinde Muliro, Danson Mwanyumba, James Gichuru, Mbiu Koinange, Kungu Karumba, Bildad Kagia, Fred Kubai, Maalim Mohamed, Mengo Woresha, Ronald Ngala miongoni mwa wengi waliokuwepo mapangoni.

Muda mfupi baada ya Jomo Kenyatta kuwasili Taita, aliyekuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitafuta njia pia hadi kuwasili akisindikizwa na rafiki yake wakati huo, Jaramogi Oginga Odinga. Hawa wote ni wanasiasa waliolemea mrengo wa siasa ya mkono wa kushoto (Communist) ilhali hata wakati huo wakiwa Taita, walitofautiana vikali kimaadili ambapo Jomo Kenyatta yeye alikaa kwa pango lake pekee yake maarufu siku hizi kama Capitalist Cave (la siasa ya mrengo wa mkono wa kulia).

Charles Mlekenyi anatueleza kwamba kunayo mapango mawili ya kihistoria. Moja ni pango la Capitalist Cave ambalo Kenyatta na wenzake waliopendekeza ama kuamini siasa ya mkono wa kulia walitumia kupanga mikakati yao. Lingine ni lile pango la Cammunist Cave ambalo washirika wa siasa ya Uchina (Mwalimu Julius Nyerere) na Jaramogi Oginga USSR (Russia) walimokuwa wakipanga mikakati yao. Nyerere alimtembelea Kenyatta mafichoni kuja kupata maarifa zaidi ya kukabiliana na Wazungu (Wajerumani waliokuwa wakitawala Tanganyika) akifahamu wazi, mwenzake amekuja na ujanja kutoka Uingereza.

WEMA WA UHURU KENYATTA

Laiti kama siyo kuchaguliwa tena kwa Uhuru Kenyatta kama rais wa Kenya mwaka 2013, bila shaka hakuna Mkenya ama Mpwani ambaye angepata kuifahamu familia maarufu na shujaa nchini ya Mzee Zephania Nyambu Mwakio na mkewe Silvia Manga Mwakio kutoka kijiji cha Mwanguwi, umbali wa karibu kilomita tatu kutoka mji wa Wundanyi, kaunti ya Taita Taveta.

Kwa wale ambao hawamjui Zephania Nyambu na mkewe Silvia, wajue leo kwamba Wakenya wote leo hii na hata Afrika Mashariki ya Tanzania na Uganda, wanasherehekea ama kutafuna matunda ya uhuru leo hii kwa sababu ya wema wa Wataita hawa wawili.

Katika ziara yake ya kwanza katika kaunti ya Taita Taveta, Rais Uhuru Kenyatta alitambulishwa Mama Silvia Manga na Mzee mmoja wa Njavungo, Mzee Ronald Mwasi. Akisalimiana naye kwa mkono, Uhuru alivutiwa na unyenyekevu na ujasiri wa mama huyu aliyekuwa na umri wa zaidi ya miaka 100. Ni wakati huo ambapo mama Silvia alimpasulia mbarika kwamba, angekuwa na roho mbaya, hata yeye hangezaliwa kwani ogopa mama anayekupikia chakula kila siku.

Kwa huruma na upendo, Rais alimuuliza chochote ambacho mama angependa kufanyiwa. Kulingana na Mzee Ronald Mwasi ambaye alikuwepo papo hapo, mama alimwambia Rais kuwa atakufa ameridhika iwapo atajengewa nyumba nzuri, apewe mifugo ya maziwa, apate gari la kumpeleka kanisani kila anapohitaji maombi na kanisa lake la Silvia Manga Church, pia lipatiwe gari la washirika na pasta wao.

MATAPELI WALIODHULUMU MAMA

Bila kupoteza muda, Rais yafahamika alimwaagiza mara moja mtumishi wa utawala wa serikali ya kaunti wakati huo kufuatilia mara moja. Maafisa husika wa serikali pia waliamrisha kufuatilia jambo hili na kuhakikisha kwamba mama amefanyiwa kama ilivyoagizwa. La kusikitisha ni kuwa mama leo hii shahidi wake ni Mungu na mtoto wake Charles Mlekenyi aliyebaki nyuma kwamba pesa ambazo aliwahi kupokea baada ya agizo la Rais ni shilingi 25,000 pekee yake kutoka kwa mkuu wa utawala aliyepewa amri wakati 2013-2914.

Mwanasiasa mmoja wa Taita Taveta na mkaribu sana wa Rais hali kadhalika anapachikwa lawama na familia ya Mzee Zephania Nyambu kwa kukwepa agizo la Rais Uhuru Kenyatta mara nyingi kwamba awapeleke wazee wa Njavungo na mmoja wa familia Ikulu kuona kwamba ahadi zilizowekwa zimetimizwa.

Hii siyo mara ya kwanza kwa familia hii kurushwa na watumishi wa serikali bila ya ikulu kujua. Mnamo mwaka 1978, kabla ya Rais Jomo Kenyatta kuaga dunia, alitaka kumzawadi rafiki yake Zephania kwa zaidi ya ekari 2000 na chungu nzima ya mifugo na mali nyinginezo ambazo alimunulia kwa kupitia ule mradi wa fidia za mashamba ya wazungu.

Alipomuuliza mwanasiasa Eliud Mwamunga (marehemu) kama angemletea mzee Nyambu ikulu ya Mombasa, alistaajabu kuambiwa na Mwamunga kwamba Zephania Nyambu alifariki kitambo cha miaka ya 1960s kumbe ni uongo na wivu tu wa kijamii. Kulingana na Mlekenyi, anasema babake alikufa na masikitiko makuu kutoka kwa kisa cha mwaka 1978 mnamo Agosti.

Anasema baada ya Jomo Kenyatta kudanganywa na Mwamunga kwa miaka kadha kwamba rafiki yake amefariki, alimpata Spehen Mwaisaka na kusisitiza kujua ukweli iwapo kweli, Zephania aliaga. Yaaminika Jomo hakuamini aliyoambiwa na Mwaisaka kwamba Zephania bado yupo.

Mlekenyi anasema anakumbuka vyema mwaka 1978 ambapo Stephen Mwaisaka aliagizwa na Rais wa kwanza kuja kumchukua Mzee ampeleke kukutana naye Ikulu ya Mombasa. Kabla ya kusafiri hadi Mombasa, Zephania alishauriana na mkewe Silvia na mwanawe Mlekenyi kwamba zawadi ya shamba na mali aliyotengewa na Rais ni faida ya urafiki mwema na afueni kwao.

Kwa kuwa wa moja ni wa moja hata akipangiwa mbili, Zephania alikufa na ugonjwa wa mawazo mnamo mwaka 1993 baada ya kufanikiwa kufika Mombasa wakati huo (Agosti 1978) n ahata kuwasiliana na rafiki yake kwa mara ya kwanza tangu 1952 wote wakamatwe, Zephania akisukumwa Shimo la Tewa kwa miaka 8 naye Jomo Kenyatta na wenzake wakisukumwa Kapenguria.

Wakati Kenyatta alipoambiwa na mkuu wa mkoa Eliud Mahihu kwamba Zephania amefika, alimwagiza kumsubiri aende kuhutubia mkutano wa Kwale kwanza ndipo akirudi jioni ile, waweze kukutana na kutafakari juu ya kuzawadiwa kwake. Ni wakati na siku ile ile ambayo Jomo Kenyatta alizuaa akihutubia mkutano wa hadhara katika shule ya msingi ya Msambweni (Bomani siku hizi ni Jomo Kenyatta Primary School) na kuanguka kabla ya kuaga dunia.

Jomo Kenyatta aliaga dunia baada ya kuanguka Msambweni huku rafiki yake wa dhati Zephania Nyambu Mwakio akimsubiri mjini Mombasa. Baada ya hapo Zephania hata mtoto wake Mlekenyi anasema hawakuwa na la kusema ili kuishi na kidonda cha roho milele.

“Baba alifariki mwaka 1993 na kidonda cha roho. Baadaye tulipata tumaini kufuatia kukutana kwa mama Silvia Manga na rais Uhuru Kenyatta mnamo 2013/14 na tukaona mwangaza tena kwamba angalau tutrakumbukwa lakini pia, mama amekufa na kidonda cha roho tena mwaka 2015 baada ya kupunjwa tena na wanasiasa na watawala wa serikali” amalizia Mlekenyi ambaye anasema maombi yake ni kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kipindi chake cha urais kukamilika.