Kwani Musalia Mudavadi ni debe tupu la 2022?

Kiongo wa ANC Musalia Mudavadi

Shida ya Musalia Mudamba Mudavadi (MMM) ni moja tu: ni kisu cha mgema ambacho, baada ya kunyanyuliwa juu minazini kileleni, huishia kutupwa sakafuni bandani kungoja ya kesho.

Maneno yake msumari kwenye siasa, lakini hana undovu wa James Orengo, unyati wa Martin Shikuku na usimba wa Karisa Maitha.

Si wengi uswahilini jinsia hii na akipatikana , watu humgeukia na kumuita ‘domo kaya’ , ‘kinangunangu’ ama ‘cherahani cha meno’.

Ndivyo alivyo M.M.M wetu….maneno mengi kama kitabu yasiyoisha na yakiisha huishilia ndiko siko ama ndivyo sivyo.Hunikumbusha kisa cha kijana mmoja mdogo Ulaya aliyeuwa wazazi wake wawili kisha akamtaka hakimu amuhurumie kwa vile sasa ni yatima!

Majuzi wakati Mudavadi alipozuru pwani alirepuka kama karabai cheteni akituhumu njama za kuliuzia shirika la taifa la usafiri wa meli (National Shipping Line) bandari hiyo kuu ya Mombasa (KPA) kinyume cha akili na katiba.

Kidole chake cha shahada kilielekea mustatili wa serikali ya Jubilee lakini masabasi wa siasa nchini wanamdhania lengo na madhumuni yake ni kuwachafulia bahari mwenyekiti wa Orange Democratic Party al maaruf ODM Raila Odinga na Naibu wake Gavana Hasan Joho ambao ni kama kwamba walishindwa kuwa wa mwanzo kupasua mtapa huo ilihali pwani ni ngome kuu ya upinzani tangu mstaafu Rais Moi kurudisha mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Huku si kutetea raslimali ya taifa ama maslahi chuma ya wapwani: ni firifinyange ya wazi za gogwe hilo la Amani National Congress (ANC) kutoka mkoa wa magharibi kuwapakazia wakunga hao wakuu wa ODM  waonekane majuha Kalulu wanaojali tagaa na matunda ya ‘handisheki’ kulikoni mzimile huo wa nchi.

Nani asiyejua bandari ndio mdomo wa Kenya na nchi za maziwa makuu? Kwanini mbunge huyu wa zamani wa Sabatia (na wakati mmoja waziri wa fedha na makamu wa Rais) asafiri hadi Mombasa kumwaga fitina bila sufuria ya ushahidi?

Yanikumbusha msaragambo wa wanasiasa na waandishi habari fulani nchini waliopiga vikorokombwe eti bandari ya KPA imewekwa rehani na serikali ya Uhuru kupata mabilioni ya mchina kujenga reli ya SGR Mombasa hadi Kisumu.Yalikuwaje ? mbona kimya kama kaburi la Abunuwasi?

Hakuna kinachomzungusha Musalia Mudavadi kote nchini akitowa cheche za maneno dhidi ya Raila na serikali isipokuwa uchu wa kuvalishwa rasmi kisibao cha kiongozi ‘halisi’ wa upinzani aliyebakia baada ya Muungano wa vyama pinzani National Super Aliance (NASA) kusambaratika kufuatia kinara wake Raila Odinga kukubali kufuturu sahani moja na Rais Uhuru Kenyatta  wa Jubilee Alliance.

Ni fungate ya Mei 9, mwaka jana iliyomtia kitumbo –mimba Mudavadi baada ya yeye na akina Moses Wetangula (Ford-K) na Kalonzo Musyoka (Wiper Party) kupigwa chenga ya steki na Mwenyekiti huyo wa NASA/ODM.

Chenga hii iliyomfanya Raila na Uhuru kusuhubiana baada ya vurugumechi katika uchaguzi mkuu uliopita 2017.Kwenye kamusi ya Mudavadi, Raila ni msaliti nusu mkate.Huwezi kupinga mwenyeji (serikali) wakati umgeni wa kulala na kuamka-abadan!

Sera ya Mudavadi ndani na nje ya nguzo ya serikali inatuzalia sinema ya msomi mwenye tajriba na karatasi zote za elimu-fedha asiye na msimamo wala pakiti ya aibu usoni.

Lau si kutemwa na kudhalilishwa na Marais Moi na Kibaki mtawalia , hangeingia dungu la upinzani.Hizi ni siasa za hasira, kisasi na unafiki zilizomjenga kinara huyo wa ANC na kumuweka peupe mataani bila ya mwelekeo wala bahati kwenye Jamhuri hii yenye umri wa miaka 56.

Je, nini ramli juu ya kiongozi huyu aliyejitenga na wawindaji wenzake porini kwa tamaa ya kigwiri mbele ya wapiga kura katika mikoa saba ya Kenya tuelekeapo uchaguzi mkuu ujao 2022? Ataweza kubeba kontena la Baba Tinga ambaye amekuwa sura ya upinzani yeye na babake Jaramogi Oginga Odinga ? Je, Mudavadi ni mgogo ama kivurugo?

Sura na buruji ya Jamhuri ya tano ijayo haitategemea unyende na pitepite mashinani za kinara huyu wa ANC bali Naibu Rais William Samoei Ruto na Gavana Hassan Joho watakavyotamka na kucheza turufu zao nyuma ya ushirikiano mpya wa Uhuru na Raila.

Kwa upeo wa mkabala wa siasa na mahesabu yalivyo hadi sasa nchini Kenya, wajihi na kiwiliwili cha Kenya siku za usoni kabla uchaguzi ujao vitaamuliwa na maingiliano na mitazamo ya wakenya wanne-Uhuru, Raila, Ruto na Joho.

Nini atakiwa afanye Musalia Mudavadi aingie kwenye unyago wa timu hii? Amekanyaga tope na maji ufuoni baharini; Je, atadiriki kuvua nguo ajitose mzima mzima mwambani ama atasalia ‘Nassoro- Kishuhira –Mficha-Uke-Hazai ?’

Musalia ana njia tatu kujinusuru kisiasa:mosi, aungane na Uhuru Kenyatta-Bila-Ruto ; pili, amkumbatie Kalonzo Musyoka waunde kikaragosi chengine mfano wa NASA wasimame kivyao kutaka Urais/Unaibu/Uwaziri mkuu 2022-ama ajisopeke apakatwe na William Samoei Ruto (nje ya kambi ya Uhuru) kama mgombea mwenza wa mbabe huyu kutoka ‘Bonde la Ufa’.Labda la nne na mwisho: ajitoe siasa kama kina Najib Balala, Salim Mwavumo na Noah Katana Ngala.

Huenda kwa sasa Mudavadi anatumiwa na maadui wa Raila kumchafuliwa jina shekhe hilo la upinzani nchini.Hii bila shaka itakuwa furaha ya kunguru kwa Ruto ambae hapatani na Raila tangu kinara huyu wa ODM kujisopeka angavu za Ikulu.

Iwapo Ruto atatemwa Jubilee ama na Uhuru Kenyatta asipate tikiti ya kusimamia wadhifa wowote 2022 basi ni wazi kungwi hilo la bonde la ufa si dude la kukubali ufala ama unyonge ;huenda akaunda mseto wa upinzani na kuingia ngwe mpya siasani kwa mara ya kwanza maishani mwake tangu alipohitimu drafu enzi za Profesa wa siasa Mzee Moi na KANU baba bin mama.

Muungano wa Ruto –Mudavadi utakuwa tishio la ziraili kwa chama tawala na ODM: bonde la ufa na mkoa wa magharibi ndizo zenye idadi kubwa sana ya wakaazi na wapiga kura ukiachilia mbali mikoa ya kati na Nyanza.

Ingawa magharibi ya Kenya jamaa zake wanajulikana kutia ‘mayai’ kapu moja, Mudavadi ana ushawishi wa kutosha kuzowa kura za maana kuinyima ODM ama chama tawala ushindi wa alfajiri.Aidha, kuna kura nyingi za waluhya mikoa mengine.

Tatizo la Mudavadi ni pwani: tofauti ya Ruto mwenye ngangari na ngwechere ,kinara huyo wa ANC hana lugha, kumbukumbu wala pesa za kumtisha Raila na Joho 2022.

Ukweli mweupe ni kwamba Mudavadi hauziki pwani.Waswahili, wamijikenda, wataita,wapokomo , mashebe na machotara hupenda mwanasiasa ngangari wa mwaga-nimwage.Viongozi wote maarufu mkoani walikuwa ‘machizichizi’ wazungumzao ‘ovyo’ jukwaani na meza  za udalali siasa.

Tazama balaa: Sheikh Abdillahi Nassir, Ronald Ngala, Mekatilili wa Menza,Fumo Liyongo, Nasoro wa Reje, Chibule wa Tsumo, Omari Masumbuko, Mwashengu wa Mwachofi, Juma Boy, Karisa Maitha, Sheikh Khalid Balala, Francis Khamis, Mwakileo, Aisha Jumwa na Hassan Joho.

Hii inatokana na usugu na kumbukumbu nrefu na katili ya kuvamiwa na kupambana na wayunani, wagiriki, wachina,warumi,wafursi, wareno , waarabu na waengereza.

Kwa wenyeji mashujaa wa maneno na vitendo hupewa taadhima zote kwa vile huwatumainisha kupata suluhu za sasa na historia kupitia kwao.Si ajabu Raila kuzowa kura nyingi sana za uraisi mkoani chaguzi zote nne zilopita.

Kutegemea Musalia Mudavadi (na hata Wiliam Ruto) ataweza kumpiku kisiasa Baba Tinga mwenye balagha za vitendawili na makovu ya ukombozi nchi leo hadi mfondogoo na kabla na baada kipute cha 2022 nchini Kenya ni kutegemea mlima Kilimanjaro kushindana na kichuguu cha mchwa.Kama hamuamini,muulizeni Rais Uhuru Muigai Kenyatta……… na Daniel Toroitich Arap Moi.