IEBC yawataka wabunge kupitisha bajeti


Na Beatrice Maganga
NAIROBI, KENYA, Ikiwa imesailia miezi michache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, Tume ya Uchaguzi, IEBC imetoa wito kwa bunge kusuluhisha suala la bajeti ya tume hiyo haraka iwezekanavyo.
Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Ezra Chiloba amesema licha ya tume kuwasilisha makadirio yake ya kima cha shilingi bilioni 31 ya kuandaa uchaguzi huo, bunge halijawasiliana na tume hiyo kuhusu mapendekezo yake.
Chiloba amesema kufikia sasa IEBC imepokea shilingi bilioni 19 pekee. Hata hivyo ameeleza matumaini kwamba  zilizosalia zitatolewa kwa wakati.
Wakati uo huo, amesema IEBC imeanza upya shughuli ya kutoa kandarasi za uchapishaji karatasi za kura baada ya mahakama kufutilia mbali tenda iliyopewa kampuni ya Al Ghurair ya Dubai.
Chiloba alikuwa akizungumza wakati wa warsha ya makamishna wa tume iliyoandaliwa katika hoteli moja mjini Niavasha. Warsha hiyo ilihudhuriwa na maafisa wengine wa uchaguzi kutoka mataifa ya Afrika Kusini, Namibia, Nigeria na Ghana.

 

Related Topics

IEBC Ezra Chiloba