Viongozi wa upinzani wahudhuria sherehe za Mashujaa

Na Suleiman Yeri

Kwa kipindi kirefu, viongozi wa upinzani wamekuwa wakisusia hafal nyingi za kitaifa hasa wakati wa utawala wa Jubilee. Lakini leo hii vinara wawili wa CORD Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula walihudhuria sherehe za Mashujaa kwenye Kaunti ya Machakos huku Kalonzo akitumia fursa hiyo kuwasuta wanasiasa waliokihama chama chake cha Wiper na kujiunga na Jubilee.

Hatua ya Kalonzo na Wetangula kuhudhuria sherehe hizo ilikuwa ishara ya kutimiza ahadi yao ya kutoandaa sherehe sambamba za mashujaa. Kalonzo alitumia fursa hiyo kutangaza kwamba kamwe vyama tanzu vya muungano wa CORD  havitavunjwa. Aidha amejipigia debe akisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais, atatokomeza ufisadi kwa vile Rais amekiri kushindwa.

Vilevile alitumia fursa hiyo kuwasuta wabunge Kisoi Munyau wa Mbooni, Joe Mutambu wa Mwingi ya Kati na Francis Mwangangi wa Yatta waliohamia Jubilee.

Akihutubu wakati sherehe hizo, mwenyeji wa sherehe za mashujaa mwaka huu ambaye ni Gavana wa Machakos Alfed Mutua  amesema ufisadi umekuwa chanzo kikuu cha ongezeko la umaskini nchini na kusema kuwa kuna haja ya Wakenya wote kushirikiana katika kuukabili.

Hata hivyo amesema chama chake cha  Maendeleo Chap Chap Chama  ki tayari kushirikiana na chama cha Jubilee ili kuhakikisha Wakenya wote wanapata maendeleo.

Kinara wa CORD Raila Odinga hakuhudhuria sherehe hizo kwani ameelekea Uingereza kukutana na wanafunzi, wasomi, maafisa wa umma na viongozi wa kisiasa katika Chuo Kikuu cha Metropolitan jijini London.