×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu:Mapinduzi ya umma yananukia Kenya

News
 Wana CORD walipokabiliana na polisi nje ya afisi za IEBC Aprili 25. Mapinduzi yanabisha hodi nchini,kwani serikali imefeli kuwahudumia Wakenya ipasavyo Picha: Jonah Onyango/Standard

Mbiu ya mgambo imelia na ishara ya kungolewa kwa viongozi wang’ang’anizi Kenya imewadia.

Mapinduzi ya umma yameanza kunukia Kenya. Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake William Ruto wamekalia kuti kavu kwani wananchi hawataki ufalme ama usultani bali wanataka demokrasia inayozingatia ukomo wa madaraka.

Ikiwa wawili hawa watazidi kutawala wakenya kwa misingi ya kikabila, chuki, ufisadi na dhulma, basi joto la kisiasa halitawaacha salama kwa maana wimbi la mabadiliko litawafagia mmoja baada ya mwingine kuelekea 2017.

Walipoingia madarakani kupitia uchaguzi uliokemewa, Uhuru na Ruto walionekana kuwa wawakilishi wa kweli wa wananchi. Lakini polepole wawili hao walianza kuvunja miguu Kenya na wakenya ili waendelee kutawala huku wakionekana kuunda serikali ya ki-imla itakayonyamazisha kila sauti ya haki na mabadiliko.

Tabia kama hizi ndizo zilizoanzisha mapinduzi ya umma kule Burkinafaso, Libya, Misri, Burundi, Brazil miongoni mwa mataifa mengine barani Afrika na hata maeneo mengine duniani.

Mapinduzi ya amani ya kuwaondoa viongozi wanaotaka kutawala kwa mabavu. Dalili sasa zinaonyesha wazi kuwa Kenya yafuata mkondo huo wa kuunda Tahrir yao na kutaka uongozi mpya baada ya kupoteza imani na serikali iliyopo.

Yaliyojiri katika jumba la tume ya uchaguzi huru ya IEBC ni ishara tosha kuwa wakenya wamechoka kupiga kura na kupokea matokeo yasiyo ya kweli.

Tahrir yanukia Kenya kutokana na kufeli kwa serikali kuwahudumia wakenya. Vijana wengi waliojitokeza kufanya maandamano ya amani nje ya jumba la IEBC ni vijana wasio na kazi na waliosahaulika na serikali inayowaajiri wazee.

Hali inazidi kuwa ngumu Kenya. Mjini Mombasa vijana wanauawa na kutoweka katika hali isiyoeleweka kila kukicha huku viongozi wa dini wanauawa kwa misingi butu ya ugaidi.

Ajira imekuwa haba, njaa yabisha hodi huku ushuru waliotoa wakenya ikiibiwa. Sakata ya NYS imesahaulika kwa maana wahusika hawatoki upande wa upinzani.

Huko Garissa, Wajir na Mandera ni vilio kila kukicha. Mauaji ya kinyama, dhulma na ukosefu wa usalama.

Nyanza chuki ya tangu na enzi ya hayati Jomo Kenyatta bado inazidi kuendelezwa. Wana-nyanza hawapati maendeleo kwa sababu ya kuwa na upinzani. Nyanza imesalia uchi na kudharauliwa.

Nairobi ni jiji la dhulma, sheria ni kwa maskini tu. Kila kukicha ni wizi, hamna usalama. Visa vya ugaidi vimelemaza biashara. Kila kitu kimesimama. Bonde la ufa na eneo la kati ni ndoa ya kudanganyana — wanafanya mapenzi ya wizi huku wakiangaliana kwa jicho la kila mmoja kutaka kumtia mwenzake mimba kabla ya kutiwa.

Isiolo, Marsabit na Moyale sio Kenya tena, sawia na Ukambani.

Wakenya wana hasira. Vijana wameamka na sasa wanataka nafasi yao. Rais Uhuru na ndugu Ruto wanakuza matatizo ya siku za usoni iwapo hawataleta mabadiliko. Ole wenu viongozi mnaotaka kutawala kwa mabavu. Ukweli ni kwamba nguvu ya Tahrir Kenya itakapoanza itaponza nguvu ya wahuni wachache Kenya. Ashakum si Matusi!

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles