Naibu Jaji Mkuu mteule Philomena Mwilu asema atastaafu akiwa na miaka sabini

Na Beatrice Maganga/Sophia Chinyezi

Hatua ya aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu, Kalpana Rawal kushtumu vikali kustaafishwa akiwa na umri wa miaka sabini imewekwa katika mizani leo hii huku Jaji Philomena Mwilu aliyeteuliwa kumrithi akitakiwa kueleza iwapo naye atakatalia uongozini pindi atakapofikisha umri huo. Akihojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki na Sheria, Mwilu hata hivyo amesema yu tayari kustaafu akifikisha umri huo.
Ikumbukwe kuwa Rawal alipinga kustaafishwa akiwa na umri wa miaka sabini kwa misingi kuwa aliapishwa kuwa jaji chini ya katiba ya zamani iliyoweka ukomo wa umri wa kustaafu kuwa miaka sabini na minne. Hata hivyo yeye pamoja na aliyekuwa Jaji Philip Tunoi walistaafishwa kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu.
Licha ya kukiri kuhusu kukithiri kwa ufisadi katika idara ya mahakama, Jaji Mwilu aidha amesema hajawahi kushiriki ufisadi na kwamba atafanikisha vita dhidi ya jinamizi hilo.