Sherehe za mashujaa zaadhimishwa huku wananchi wakitakiwa kudumisha amani

Na Beatrice Maganga

Kwa mara ya pili sasa katika historia ya taifa hili, maadhimisho ya shereza za kitaifa yamefanyika nje ya jiji la Nairobi. Baada ya maadhimisho ya Siku Kuu ya Madaraka kuandaliwa mjini Nakuru mwezi Juni mwaka uliopita, leo imekuwa zamu ya Kaunti ya Machakos kuandaa Sherehe za Mashujaa. Rais Uhuru Kenyatta ameziongoza sherehe hizo ambazo hazikuwa na hotuba ndefu ilivyo desturi huku akitoa ushauri wa kuendeshwa kwa siasa zinazohusu sera badala ya ukabila.

Alipochukua fursa ya kuwahutubia wananchi waliofurika katika uwanja wa Kenyatta Kaunti ya Machakos, Rais Uhuru Kenyatta aliwashauri wananchi kuwa makini uchaguzi mkuu unapokaribia na kuwachagua viongozi kwa misingi ya utendakazi.

Aidha amewapongeza mashujaa katika nyanja mbalimbali waliolifanya taifa hili kutambulika kote duniani.

Rais aidha amesema hatua ya sherehe za kitaifa kuandaliwa kwenye kaunti mbalimbali badala ya kufanyikia jijini Nairobi pekee ni dhihirisho tosha kwamba serikali yake imekumbatia ugatuzi, kauli ambayo pia ilizungumziwa na Naibu wake, William Ruto.

Ruto aidha ametaja umuhimu wa wananchi kuzingatia sera za viongozi huku akitoa changamoto kwa upinzani kujitayarisha vilivyo kwa uchaguzi mkuu ujao kwani sera ndizo zitakazowavutia wananchi wala si kabila la kiongozi fulani.

Mapema Alhamisi kabla ya kuzihudhiria sherehe za Mashujaa, Rais alizindua upanuzi wa barabara ya Machakos Athi River.

 Sherehe za mashujaa zilianza kuadhimishwa pindi katiba ya sasa ilipoidhinishwa ili kutoa fursa ya kutambuliwa kwa mashujaa mbalimbali. Awali Oktoba ishirini iliwa sikukuu ya Kenyatta.