Raila alazimika kukatiza hotuba Kericho

Wakazi wa eneo la Kapsoit katika kaunti ya Kericho wamemsuta mwaniaji wa kiti cha urais katika muungano wa NASA Raila Odinga na kumtaja kuwa mwongo anapodai kuwa kilimo biashara katika eneo hilo sasa ni duni.

Katika matangazo ya moja kwa moja ya hutuba ya Bw Odinga eneo hilo, kupitia KTN News, wananchi waliskika wakisema kuwa eneo hilo ni ngome ya chama cha Jubilee.

Kwa wakati mmoja Bw.Odinga aliposema kuwa biashara ya kilimo imeporomoka na akawauliza ikiwa ni kweli au alikuwa akisema uongo, baadhi yao waliitikia kwa kishindo kuwa ni uongo.

"Biashara ya kilimo si imeanguka,? wakulima wa mahindi, kahawa wanalia. Ukweli au uongo,?" aliuliza Bw Odinga.

"Uongo!" waliskika wakimjibu kwenye kanda hiyo.

KANDA: HOTUBA YA RAILA KERICHO


Raila kwa muda hakusita kuwaomba kura huku akisema kuwa wakulima wa mahindi, majani chai na hata kahawa walikuwa na kilio kwa kuanguka kwa sekta hizo.

Mara kadha kwenye kanda hiyo, kundi la aliowahutubia lilisisitiza kuwa si kweli kwamba sekta hizo zimekandamiza matumaini ya mafanikio ya kilimo.

Bw Odinga ambaye alikua ameandamana na gavana wa Bomet Isaac Ruto alilazimika kuacha hotuba yake na kumruhusu Ruto azungumze na wakaazi wa eneo hilo, huku gavana huyo akiwahutubia kwa lugha ya Kikalenjini .

Ruto alionekana kumpigia debe mwaniaji wa wa kiti cha wadi hiyo kupitia tikiti ya Chama cha Mashinani.

Gavana Ruto amekabidhiwa jukumu la kuhakikisha kuwa muungano wa NASA unapata sehemu ya kura za maeneo ya bonde la ufa, sehemu inayoaminika kuwa ngome ya wafuasi sugu wa Jubilee.