Premium

Wataalam washauri ushirikiano kukabili saratani ya kizazi

Wataalam katika sekta ya Afya wanatoa wito kwa serikali na washikadau wengine kushirikiana kufadhili ili kufanikisha mipango ya kutoa chanjo na ukaguzi dhidi ya ugonjwa wa saratani.

Rais wa Muungano wa Wataalam wa Afya ya Uzazi Kenya Obstetrical Gynaecological Society Kireki Omanwa amesema kuna haja kwa kuwapo kwa mpango wa kitaifa wa kuwapa chanjo wanawake na wasichana dhidi ya virusi vya Human papillomavirus HPV ili kuzuia saratani ya kizazi.

Akihojiwa katika Spice FM mapema leo, Omanwa anasema licha ya wataalam hao wa afya kushauri wasichana wa kati ya miaka tisa na kumi na minne kupata chanjo hiyo, idadi ya wanaojitokeza kuchanjwa ni ya chini mno.

Aidha amesema wanawake wanaofanyiwa ukaguzi ili kuwasaidia kugundua mapema iwapo wanaugua saratani hasa ya kizazi, ni wachache mno ambao ni asilimia 5 pekee kwa mwaka, akisema hilo limechangia vifo ambavyo huripotiwa nchini.

Kulingana na takwimu watu 42, 000 hugunduliwa kuugua saratani nchini kila mwaka, huku saratani ya matiti ikiongoza ikifuatwa na Saratani ya Kizazi. Aidha wanaofariki dunia zaidi ni wanawake wanaougua saratani ya kizazi, huku wanawake 3, 200 wakifariki dunia kila mwaka, kumaanisha wanawake tisa hufariki dunia kila siku kutokana na saratani hiyo ya kizazi.