Wakili Paul Gicheru wa ICC, ameaga dunia

Wakili Paul Gicheru, ambaye alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kuhitilafiana na mashahidi katika kesi za Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ameaga dunia.

Wakili Gicheru alipatikana Jumatatu jioni nyumbani kwake Karen Nairobi akiwa ameaga dunia.

Polisi na familia yake wanaamini kwamba Gicheru alizimia na kuaga dunia huku wakikosa kutoa taarifa zaidi kuhusu kifo chake.

Wakili Gicheru alijisalimisha ICC Novemba mwaka 2020 baada ya kuepuka kukamatwa kwake kufuatia agizo lililotolewa mwezi Machi mwaka 2015.

Gicheru alidaiwa kuhusika katika kuwashawishi mashahidi katika kesi dhidi ya aliyekuwa Naibu wa Rais wakati huo William Ruto, Mwanahabari Joshua Arap Sang vilevile Henry Kosgey ambapo ICC ilikosa kuthibitishia mashtaka dhidi yao Januari mwaka 2012.

Gicheru ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 52.