Mada hii tayari imekutia kichefuchefu. Unavyodhani sivyo, bali ninamaanisha kuwa mapenzi ni sawa na kohozi yakitoka hayafichiki. Naanza kwa kusema kupenda si kosa, kosa ni kulegea kimapenzi na kuwa mwanamume anayeyumbishwa na makalio. Leo nazungumzia mapenzi ndani ya NYS. Baada ya kusikiza wimbo wa Sura Yako uliotungwa na Sauti Sol, nauliza mnijibu enyi Wakenya wenzangu mlio na elimu; Anne Waiguru amekalia chapati ya nani ndipo hachukuliwi hatua za kisheria? Bila shaka, suala la Waiguru si kukaliwa chapati kama walivyoimba Sauti Sol bali ni kukaliwa sima!
Majuzi ripoti ya Ipsos Synovate ilisema kuwa aliyekuwa waziri wa ardhi Charity Ngilu, naibu rais William Ruto na waziri wa ugatuzi na mipango ya taifa Anne Waiguru ni miongoni mwa viongozi waliofikiriwa kuwa wafisadi na Wakenya. Kwa mujibu wa mtafiti mkuu wa Ipsos, Tom Wolfe, asilimia 50 ya Wakenya walikuwa na ufahamu wa kesi ya ufisadi inayomkabili Ngilu; naibu rais Ruto akitajwa na asilimia 31 ya Wakenya na asilimia 28 wakimtaja waziri Waiguru.
Ajabu ni kwamba tofauti na Ngilu na hata baada ya wizara yake kupoteza mamilioni ya pesa, Anne Waiguru bado ni kamanda wa kike asiyeweza hata kutajwa wala kuguswa na idara ya upelelezi na wabunge.
Kati ya Wakenya waliochangia kutoa picha za fedheha nchini ni:
Ndegwa Muhoro
Afisi yake imekashifiwa vikali kutokana na utendakazi wake. Wengi wanamwona Muhoro kama mfanyabiashara na jamaa wa fursa anayejinufaisha badala ya kuwasaidia Wakenya. Afisi yake ni kama Kilabu cha mamilionea wanaowadhulumu kina yahe. Wahuni wanapora na kudhulumu hata wageni wanaowekeza humu nchini na kisha baadaye kukimbilia makao makuu ya CID kutafuta ukuruba.
Muhoro tunajua vile wageni na wakenya wanavyotapeliwa katika biashara za dhahabu, tuko jikoni na zamu yako kama sio sisi basi wanahabari wengine watawajuza wakenya. Afisi ya Muhoro ilishindwa kutatua ulanguzi wa dhahabu labda kwa sababu yeye binafsi anadaiwa kuhusika, Mauaji ya afisa wa GSU Erastus Kirui Chemorei, Mauaji ya shahidi katika mahakama ya ICC Meshack Yebei na mauaji ya viongozi wa kidini.
Kadinali John Njue
Majumba ya Mungu yamegeuzwa na kuwa soko huru la wizi, utapeli, ukabila, dhulma na siasa chafu. Viongozi wa kidini sasa hawamwogopi Mungu bali serikali. Majuzi nimemskia Kadibali Njue akisema kuwa walimu wana hila fulani wala sio masuala ya mishahara! Nimewapeza viongozi wa kidini kama Marehemu Father John Kaiser, Kadinali Maurice Otunga, Timothy Njoya na Alexander Muge. Hawa ni viongozi wa kidini waliokuwa wakiwakosoa viongozi serikalini kila walipokwenda kinyume na maandiko.
Adan Wachu
Supkem ni nini? Supkem inasimamia nani? Viongozi wa Supkem huonekana tu wakati wa siasa. Mko wapi wakati vijana wanauawa kiholela na idara za usalama? Ni Waislamu gani mnaowazungumzia kwa niaba yao? Iwapo wenzenu wanaogopa kuwaeleza mimi sitamwogopa yeyote ila Allah kwa kuwaweka sawa mnapofaa. Adan Wachu na wenzako nawakumbusha kuwa kesho mbele ya Mungu mna mengi ya kujibu. Tumewaona mashekhe wa msimu, mashekhe wa kisiasa wanaozungumza kwa niaba ya tumbo zao kwa kisingizio cha kuzungumza kwa niaba ya Waisilamu.
Joseph Boinnet
Niliposikia umeteuliwa, nilifyatua domo kwa kuwa nilijua na kusikia katika vyombo vya habari na mitandao siasa zilizochezwa kiasi cha wewe kupata nafasi hiyo. Lakini sasa mauaji ya kiholela yanazidi kuikumba idara yako. Nikikulinganisha na aliyekuwa kamishna wa polisi Meja Jenerali Hussein Ali, nakuona kama skauti anayefuata upepo. Ashakum si matusi bwana Boinnet na kama nimekuudhi naomba msamaha.
Mugo wa Wairimu amedhalilisha mama na dada zetu, ameniita gaidi na kupasisha ujumbe wa mimi kuuawa. Nimeripoti katika kituo cha polisi cha central kupitia maafisa wako kwa jina la Biyegon, Joyce na Sajenti Ringera, sio Mugo wa Wairimu pekee bali pia afisa mwengine wa idara ya magereza, lakini maafisa wako hawatambui haki ya mnyonge dhidi ya wenye nchi. Si-ripoti tena maana nimejua wazi kuwa usalama kwa wote ni usalama kwa wenye mapeni.
Kanyari hajachukuliwa hatua na kesi ya Ng’ang’a kabla ya kukamatwa iliibua maswala. Polisi wako wanaojiita flying squad, Subaru, scorpion, anti-kidnapping na anti-terror wanadaiwa kupora na kuua vijana wasio na hatia. Majuzi shirika la kutetea haki za binadamu KNHCR liliwakashifu maafisa wako wanaoua bila huruma wakijifanya kupiga vita ugaidi. Aidha utafiti wa Ipsos ulibainisha kuwa mauaji ya kiholela yamekithiri katika maeneo ya kaskazini mashariki ya Kenya. Wewe umesalia kimya na ndio nitasema Mungu atazifadhili familia za wote walioathiriwa.
Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi, KTN. Wasiliana naye kupitia [email protected], [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, ama Twitter: @mohajichopevu