Atwoli ndiye mpasua mwamba wa 2022

Katibu mkuu wa vyama vya wafanya kazi nchini COTU Francis Atwoli.

Ishara ya mtego wa kutegana wa NASA ni dhahiri uliteguliwa punde tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kukumbatiana kwa busu la mkono wa kheri, almaarufu “hendisheki”.

Uhusiano mpya baina ya Rais wa Jamhuri na kinara wa upinzani ulizika kabisa katika kaburi la sahau maazimio ya ushirikiano wa vyama vya ANC (Musalia Mudavadi) na Ford Kenya (Moses Wetangula) ambao wote hawa wanajivunia kumchangia kura za urais Raila Odinga kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita wa 2017.

Mshirika mwingine wa kisiasa Stephen Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper kamwe hatuna nafasi ya kumzungumzia sana hapa kwa kuwa kila mmoja wao wanamuelewa kwamba alama yake ni mwavuli ambao wakati wowote unaweza kupeperushwa na upepo mkali wa kisiasa kama ilivyo kawaida yake ya kuyumbayumba kimsimamo.

Kwa kifupi, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (WIPER) na Moses Wetangula (FORD KENYA) walipoteza rahamani ya siasa ya 2022 punde gwiji lao Raila Odinga stadi kwa karata ya kisiasa kuwaacha inje ya mshikamano wake mpya na Uhuru.

Kalonzo kwa kuwa hawezi kuvumilia dhiki la kuwekwa pembeni kwa muda, alifuata nyayo ya Raila kumrai Rais Uhuru Kenyatta angalau apate leu la kujisitiri kimaisha kwa kuteuliwa pia kuwa mjumbe maalum wa harakati za kuleta uwiano na amani Kusini mwa Sudan.

Nyota wa Magharib Huku viongozi hawa wawili kutoka eneo la Magharib Moses Wetangula “Weta” na kaka yake Musalia Mudavadi “MDVD” wakihangaika kutafuta mwanya wa kupenyea siasa yao ya 2022, sifa zao nchini na maeneo wanayotegemea zinazidi kudidimia.

Mabingwa ama nyota wanaojitokeza kuwa moto wa kuotea mbali kutoka jimbo la Magharibi mwa Kenya ni katibu mkuu wa vyama vya wafanya kazi nchini COTU, Francis Atwoli anayeenziwa na wengi kwao huko kijamii kama mlezi mkubwa wa siasa leo hii na Gavana Wycli­ Oparanya wa Kakamega ambaye Raila amewategea kama washirika wapya endapo MDVD na WETA wataingia mitini kabla ya 2022.

Oparanya yungali amesimama kidete chamani ODM ilhali Francis Atwoli amekuwa kama muunganishi wa viongozi wa jimbo la magharib na jamii nzima dhidi ya msimamo wa kitaifa, wa kiserikali na hususani wa kinara wa ODM.

Umoja wa jamii za Magharib zinategemea mwongozo wa nguzo moja ya kisiasa ambapo kwa miango fulani ya uchaguzi mkuu, upinzani wa Raila Odinga umeonekana kuwa mstari wa mbele kwa kuwa jimbo la Nyanza na Magharib zimeunganishwa na uhusiano wa mashemeji wa kuozana kijamii.

Azma ya Atwoli Wadadisi chungu nzima wa siasa ya kitaifa wananong’ozana kuwa katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli huenda akawa unganisho kubwa kwa jamii ya magharib baina ya upinzani na serikali kuliko vijogoo viwili vya nyanda hizi Moses Wetangula na Musalia Mudavadi.

Aliyekuwa seneta wa Kakamega, Bonny Khalwale (tunampa pole kwa kumpoteza mkewe hivi punde) tayari amekwisha jitosa kwa merikebu ya naibu rais William Ruto na ijapo anasema amehamia Jubilee, hali ingali na kiza iwapo ndicho chama kitachuchumaa mpaka 2022 ama kuvunjikia guu njiani kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wengine hali kadhalika wanazungumzia kwamba Francis Atwoli huenda akatamani ama kumezea mate wadhifa fulani wan chi lakini haya ni madai tu ambayo bado yamefunikwa.

Hii itategemea msururu wa mapendekezo yaliyoezekwa kwenye kamati inayoshughulikia marekebisho ya katiba ya BBI.

Haitakuwa jambo la ajabu endapo azimio la BBI litafauli na nafasi ama nyadhifa zaidi kuongezwa kuwaona aidha Francis Atwoli ama Wycli­ Oparanya wamefaulu kutuzwa moja wapo ya nyadhifa hizi mpya.

Wanaopenda umbea wanasikika wakitaja kwamba kumependekeza majimbo 12 ambayo yatahifadhi kaunti zake lakini kutakuwa na kiongozi mkuu wa jimbo wa kuwamwilika magavana na uchumi wa kaunti.

Oparanya vs Atwoli Wakereketwa hapa wananena kuwa ikiwa jimbo la kusimamia kaunti kulingana na mapendekezo yasemwavyo litakuwa, basi kunao uwezekano mkubwa wa mmoja wao, aidha Atwoli ama Oparanya mmoja anaweza kuezekwa hapo na mwingine kuangaliwa wadhifa wa kitaifa kwenye mgao wa kitaifa unaotarajiwa kuletwa na mapendekezo ya kamati kuu ya BBI.

Kwa kweli, hawa nyota wawili sasa hivi ndio wanaobobea katika safu ya magharib baada ya Musalia Mudavadi na Moses Wetangula kuonekana kuchanganyikiwa tangu kuboreshwa kwa uhusiano baina ya kinara wa upinzani na Rais Uhuru Kenyatta.

Uhasama unaojitokeza sasa baina ya Mudavadi na Raila, unawakumbusha wakenya mwaka 2012 ambapo viongozi hawa walibumburushana kisiasa na hali hiyo kumpa nguvu Uhuru Kenyatta na William Ruto kuwabwaga uchaguzini.

Tetesti zinajitokeza kwamba malumbano ya ODM na ANC yamepashwa misuli upya na kinyang’anyiro kinachoendelea cha uchaguzi mdogo wa Kibra, mgao wa fedha za vyama zinazong’ang’aniwa na muungano wa NASA na Mudavadi kudai kwamba aliachwa usingizini wakati Raila Odinga akielekea jengo la Harambee kwa “hendisheki”.

Francis Atwoli na Wycli­ Oparanya yaonekana wazi wanachekelea bafuni afro-sinema inayoeendelea huku wakifahamu wazi kwamba vita vya kunguru angani humsaidia samaki kuangukia na angaa kipande cha nyama!