Serikali imetangaza mpango wa kuufufua uchumi; Ksh53.7B zimetengwa

Serikali imetangaza mpango wa kuufufua uchumi ambao umeendelea kudorora kufuatia maambukizi ya virusi vya korona. Rais Uhuru Kenyatta amesema shilingi bilioni hamsini na tatu zimetengwa kufanikisha mpango huo kwa kuangazia mambo manane muhimu.

Sekta ya muundo msingi imetengewa shilingi bilioni tano  zitakazotumika kuwaajiri wafanyakazi wa humu nchini kufanikisha ukarabati wa barabara ambazo zimeathirika kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha. Fedha hizo zitatumika katika ukarabati wa Barabara na madaraja.

Kuhusu Elimu, jumla ya walimu elfu kumi wataajiriwa na wataalamu elfu moja wa teknolojia ili kuimarisha mafunzo kwa wanafunzi wanaoendeleza masomo kupitia mtandao, baada ya shule kufungwa kufuatia maambukizi ya Korona.

Ili kufanikisha mpango huo Wizara ya Elimu itapokea shilingi bilioni 6.5.

Aidha mazungumzo yanaendelea kuhusu hatua zaidi zitakazochukuliwa katika sekta hiyo.

Rais amesema kipato cha wafanyabiashara wadogowadogo kimeathirika pakubwa akisema wametengewa shilingi bilioni tatu kwa mikopo. Aidha bilioni kumi na tatu zitatolewa kulipia madeni ya kodi, wakati ambapo  Wizara ya Afya tayari  imetoa bilioni thelathini  kuwasaidia kulipa madeni mengine.

Serikali pia inaendelea na mpango wake wa kutekeleza huduma ya afya kwa Wote, huku rais akisema wahudumu elfu tano zaidi waliohitimu na vyeti pamoja na diploma wataajiriwa kwa kandarasi ya mwaka mmoja. Shilingi bilioni 1.7 zitatolewa kwa sekta ya afya ili kuongeza vitanda kwenye hospitali ya umma kuwashughulikia wagonjwa.

Sekta ya Kilimo ambayo ni uti wa mgongo itapata shilingi bilioni 3 zitakazotumika katika ununuzi wa pembejeo kwa wakulima wenye mashamba madogo elfu mia mbili.

Sekta ya maua ambayo imeathirika zaidi itapata shilingi bilioni 1.5. Sekta nyingine zilizofanywa kipau mbele katika mpango huo wa serikali ni Utalii pamoja na viwanda.