Gavana Sonko kumzawadi mwenye taarifa kuhusu mwanamke aliyedhulumiwa.

Gavana wa Nairobi, Mike Sonko ametangaza zawadi ya shilingi elfu arubaini kwa yeyote mwenye video iliyomnasa mwanamke akimnyonyesha mwanawe, alipokuwa amebebwa katika gari la maafisa wa kaunti hiyo.

Kupitia mtandao wake wa Facebook, Sonko amesema mwanamke huyo anadaiwa kukamatwa na kulazimishwa kuketi juu ya gari hilo na maafisa wa Kaunti ya Nairobi kabla ya kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Central.

Dereva wa gari hilo amepinga madai hayo akisema, gari hilo lilikuwa limeegeshwa nje ya kituo cha wazima moto, na wakaelekea kwa chakula cha mchana na waliporudi wakamkuta mama huyo juu ya gari hilo akimnyonyesha mwanawe.

Hata hivyo Sonko ameahidi kuchukulia kwa hatua kali za kisheria dhidi ya maafisa waliohusika kwenye tukio hilo iwapo watabainika kuwa na hatia.