Mshukiwa wa mauaji Monica Kimani ,Joseph Irungu, kubaini kwa kipindi cha wiki mbili iwapo ataachiliwa kwa dhamana ama la

Mshukiwa wa mauaji ya mfanyabiashara, Monica Kimani Joseph Irungu, maarufu Jowie, atabaini kwa kipindi cha wiki mbili zijazo iwapo ataachiliwa kwa dhamana ama la. Jowie aliwasilisha rufaa mahakamani akitaka ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana litathminiwe upya baada ya mahakama kulipinga ombi jingine sawa na hilo miezi sita iliyopita.

Mshukiwa huyo amesisitiza kwamba hakuhusika na mauaji ya Monica mnamo mwezi Septemba mwaka uliopita katika makazi yake kwenye Mtaa wa Kilimani, jijini Nairobi.

Jaji James Wakiaga ameagiza kwamba ombi la mshukiwa lisikilizwe tarehe 21 mwezi huu. Aidha Jaji Wakiaga ameuagiza upande wa mashtaka kumkabidhi mshtakiwa taarifa zote kuhusu kesi dhidi yake. Ombi lake la awali lilikataliwa kwa misingi kwamba huenda angehitilafiana na mashahidi ama hata kusafiri nje ya nchi. Aidha mahakama ilisema huenda angehitaji ulinzi mkuu ikizingatiwa anatuhumiwa kujipiga risasi begani ili kuficha ukweli kuhusu mauaji ya Monica.

Ikumbukwe alishtakiwa pamoja na mpenziwe ambaye ni Mwanahabari, Jacque Maribe japo mwanahabari huyo aliachiliwa huru kwa dhamana ya shilingi milioni moja pesa taslimu ama shilingi milioni 2.