Muhubiri akamatwa Malindi kwa kuuchochea umma dhidi ya kusajiliwa kwa Huduma Namba

Maafisa wa polisi mjini Malindi wamemkamata Muhubiri kwa jina Paul Makenzi kwa kuuchochea umma dhidi ya kusajiliwa kwa mfumo wa kidijitali wa NIIMS.  Polisi wanadai mshukiwa aliuchochea umma kutosajiliwa katika kipindi kilichopeperushwa katika kituo cha runinga cha Times akidai kuwa nambari ya Huduma Namba wanayopewa Wakenya baada ya kusajiliwa ni ya kishetani.

Katika kipindi hicho alichokiita ''End Times'' muhubiri huyo aliihusisha huduma namba na ile ya 666.

Maafisa wa Idara ya Upelelezi DCI na wale na Bodi ya Kuthibiti Filamu nchini KFCB walifanya msako katika kanisa la  Good News International lililoko Mlaindi na kuchukua kamera, compuyuta na kanda za video.

Meneja wa KFCB eneo la Pwani Bonventure Kioko amesema wana idhini kuendelea kumzuilia mshukiwa katika kituo cha polisi cha Mlaindi kwa siku 21 huku uchunguzi ukiendelea

Si maa ya kwanza kwa muhubiri huyo kukamatwa, mwaka 2017, yeye pamoja na mkewe Joyce Mwikamba walishtakiwa kwa kuendeleza mafunzo ya itikadi kali.