Waziri Matiang’i amekuwa sugu toka utotoni

 
Waziri wa Usalama wa Taifa na Ushirikishi wa Serikali Kuu Dkt Fred Matiang’i.

Wakenya leo hii wamemheshimu Waziri wa Usalama wa Taifa na Ushirikishi wa Serikali Kuu Dkt Fred Matiangí kama mpasua mwamba katika masuala sugu ambaye kwa njia moja au nyingine, serikali imeelekea kufikia ngamani mwa suluhisho.

Yeye ni kimbunga ambacho ukisimama mbele yake, utasombwa na kikukuzi (upepo) wake mkali wa msimamo wa kikazi. Wengi hatahivyo hawajui kwamba Matiang’I sawia na Wakenya wengi, ni mtoto wa skwota ambaye wazazi waliwajibika kuhama kutoka kwa kijishamba kidogo katika eneo la Mugirango Kusini hadi eneo bunge la Borabu Kaunti ya Nyamira wanapoishi kwa sasa.

Nyota ya Waziri wa Usalama wa Taifa na Ushirikishi wa Serikali Kuu Dkt Fred Matiang’i inazidi kung’ara kila kukicha tangu ateuliwe kwenye baraza la mawaziri mnamo mwaka wa 2013.

Dkt Matiang’i ndiye Waziri mwenye ushawishi mkubwa serikalini kufuatia Rais Uhuru Kenyatta kumteua kama mwenyekiti wa kamati ya baraza la mawaziri inayohakikisha kuwa miradi yote ya serikali kuu inatekelezwa.

Uteuzi huo uliofanyika mnamo Januari mwaka huu umemfanya Waziri Matiangi kuwa nambari tatu serikalini nyuma yake Naibu wa Rais Dkt William Ruto na Rais Uhuru Kenyatta jambo ambalo limezua msisimko eneo la Gusii anapotoka na nchi nzima kwa jumla.

Waziri Matiangi anajivunia uungwaji mkono na viongozi waliochaguliwa katika Kaunti za Kisii na Nyamira haswa kutokana kwamba familia yake ina mzizi katika eneo bunge la Mugirango Kusini na baadaye babake mzazi aliweza kuhamia eneo bunge la Borabu Kaunti ya Nyamira wanapoishi kwa sasa.

Hata hivyo Waziri Matiangi hajatangaza hadharani iwapo angependa kujiunga na siasa au kubaki kama mtumishi wa umma baada ya mwaka wa 2022 ambapo Rais Kenyatta atakamilisha hawamu yake ya pili kama rais wa jamuhuri.

Waziri huyo alipata shahada yake ya kwanza katika chuo kikuu cha Kenyatta, na shahada za uzamili na uzamifu katika chuo kikuu cha Nairobi na ameweza kuwa mhadhiri katika vyuo vikuu vya Egerton na Nairobi kabla ya kufanya kazi na mashirika mbalimbali nchini na hata uko ulaya.

Dkt Matiangi ameweza kuhudumu kwenye benki ya dunia,muungano wa mabunge ya Jumuia ya Madola, shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa, Shirika la Maendeleo ya kimataifa la Marekani, Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Canada na mashirika mengine kabla ya kuteuliwa kama waziri.

Mwalimu ya Shule ya Upili ya Kiabonyoru katika Kaunti ya Nyamira Richard Atemba alisema kwamba Waziri Matiangi aliweza kunoa makali ya uongozi alipokuwa mwanafunzi katika Shule hiyo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Kisii kwenye kidato cha tano.

“Waziri Matiangi aliondoka shuleni mwetu mwaka wa 1984 alipokamilisha masomo ya kidato cha nne akiwa kiranja wa kusimamia mankuli ya wanafunzi ambapo alijulikana kama ‘nusu mwalimu’ kutokana na jinsi alivyotekeleza wajibu wake na kujizolea sifa miongoni mwa wanafunzi,” akasema Atemba.

Mwenyekiti wa kongomano la Wabunge kutoka jamii ya Wakisii aliye pia Mbunge wa Mugirango Kasikazini Joash Nyamoko alisema kuwa Dkt Matiangi ameiwakilisha jamii yake vyema kwenye ngazi ya kitaifa kutokana na utendaji kazi wake bora kwa miaka mitano iliyopita.

“Sina wasiwasi wowote nikisema kwamba Waziri Matiangi ndiye Waziri ambaye ametekeleza wajibu wake kwa njia bora zaidi tangu taifa letu lijinyakulie uhuru kutoka kwa wakoloni miaka 55 iliyopita na ningependa kuwaomba wenzake waige mfano wake mzuri,” akasema Nyamoko.

Mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tongi alisema kwamba Waziri Matiangi anafuata nyayo za viongozi wa kutajika kutoka jamii ya wakisii kama vile mawaziri wa zamani Simeon Nyachae, marehemu Lawrence Sagini, marehemu James Nyamweya na marehemu Zachary Onyonka.

Tongi alisema haswa Matiangi ni mwanafunzi mzuri wa Mzee Nyachae ambapo aliweza kuhudumu kama msaidizi wake na meneja wa kampeni ya Urais wakati Mzee Nyachae aliwania wadhifa wa Urais mwaka wa 2002 ambapo kwa mara ya kwanza jamii ya wakisii ilizungumza kwa sauti moja.

 “Ni wakati mwafaka kwa jamii yetu ya wakisii kusimama na Waziri Matiangi kwa vile amedhihirisha anao uwezo wa kuwa kiongozi mzuri na yeyote atakayetaka kuzungumza nasi apitie kwa Bwana Matiangi,” akasema Tongi.

Mbunge wa Bomachoge Borabu Profesa Zadock Ogutu alisema kuwa Waziri Matiangi alijivunia sifa chungu nzima miongoni mwa wakenya baada ya kulainisha sekta ya elimu nchini kwa kukomesha visa vya wizi wa mitihani.

“Juhudi zake waziri Matiangi zimewawezesha wanafunzi kwenye shule zetu za msingi na upili nchini kupata matokeo ya kweli na hivyo kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu na taasisi za anuai kwa njia rahisi kushinda ilivyokuwa hawali,” akasema Prof Ogutu.

Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka alisema kwamba Waziri Matiangi amedhihirisha kwamba anayo tajiriba ya kuhudumu kwa wadhifa mkubwa kama Rais au Naibu Rais kutokana na utendaji kazi wake bora.

Onyonka alisema kwamba Waziri Matiangi ndiye kiongozi wa hadhi ya juu kutoka jamii ya wakisii ambaye anaweza kupeanwa kuiwakilisha kwenye ngazi ya kitaifa na kwamba anajivunia uungwaji mkono mkubwa kwenye jamii hiyo.

 “Dkt Matiangi anadhihirisha hulka ya mwanamume wa jamii ya wakisii ambaye hufanya kazi zake kwa bidii, mwenye kupenda ukweli na mwenye nia ya kuhakikisha anafanikiwa katika kila jambo analotekeleza”, akasema Onyonka.

Mbunge wa Bomachoge Chache Alpha Miruka alisema kwamba taifa la Kenya linawahitaji viongozi wenye tajiriba kama ya Matiangi ilikuhakikisha kwamba liko kwenye mpangilio wa mataifa yanayoendelea kwa kasi sana ulimwenguni.

Miruka alisema kuwa Matiangi anajulikana kwa kutowatetea hata marafiki zake wanapojipata kinyume na sharia akisisitiza kwamba wakenya wanamuhitaji kiongozi wa sampuli hiyo ili kufikia upeo wa juu zaidi kimaendeleo.

 “Sisi kama wabunge kutoka eneo la Gusii tunajua kwamba hatuwezi kumwendea waziri Matiangi kwa msaada tunapojipata tumeenda kinyume na sharia, huyo ndio sampuli ya kiongozi wakenya wanahitaji,” akasema Miruka.

Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro alisema kwamba viongozi wa jamii ya wakisii wanashukrani tele kwake Rais Uhuru Kenyatta kwa kumpandishia waziri Matiangi cheo cha kuwa kiranja wa mawaziri.

 “Rais Uhuru Kenyatta aliona  uongozi bora kwa Waziri Matiangi alipobuni baraza lake la kwanza la mawaziri manamo mwaka wa 2013 ambapo jina la ndugu wetu likikuwa la kwanza kutajwa,” akasema Osoro.