Bunge la Seneti limebuni kamati ya kutatua mzozo wa kisiasa kati ya Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho na wawakilisha wadi wa bunge la Mombasa. Mzozo huo ambao ulianza wakati gavana Joho alitishia kuanzisha mchakato wa kuwatimua baadhi ya wawakilishi kwa madai ya kukosoa utendakazi wake, sasa umefika mbele ya kamati za ugatuzi na maendeleo ya serikali.
Joho ambaye anatarajiwa leo hii kufika mbele ya kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Seneta wa Laikipia John Kinyua, anatarajiwa kuweka wazi chanzo cha mgogoro baina yake na wawakilisha hao. Licha ya shughuli za maridhiano kuendelea, kiongozi huyo ameapa kuendelea na kushinikiza kutimuliwa kwa baadhi ya wawakilisha anaowataja kuwa waasi na maadui wa maendeleo.
Kwa upande mwingine, Joho amelaumiwa na wawakilishi hao kwa kuzembea na kutelekeza majukumu yake akiwa gavana, suala ambalo amepuuzilia mbali akilitaja ni njama ya kumlenga visisyo. Kamati hiyo vilevile imemualika spika wa bunge la Mombasa Aharub Khatri, kutoa mwanga zaidi kuhusu mzozo huo ambao umetishia kusambaratisha huduma za maendeleo kwenye kaunti ya Mombasa.