Balozi wa Uingereza humu nchini asema wahusika wa ufisadi nchini wanafaa kufungwa jela

Rais Uhuru Kenyatta tayari amewasili kwenye ukumbuki kunakoandaliwa kongamano la sita la ugatuzi kwa uzinduzi rasmi.  Baadhi ya viongozi ambao wamehutubu wakati wa vikao vya asubuhi vya kongamano hilo wamelizungumzia suala la ufisadi.

Akihutubu kwa niaba ya maseneta, Seneta wa Siaya, James Orengo amesema hatua ya kuwakamata washukiwa haitoshi kudhihirisha kwamba vita hivyo vimeimarishwa. Orengo amesema wahusika wanastahili kuwajibishwa bila kujali hadhi yao katika jamii.

 

Kauli sawa na hiyo imetolewa na Balozi wa Uingereza humu nchini, Nic Hailey ambaye amesema imani ya Wakenya katika vita dhidi ya ufisadi itaimarika iwapo tu wahusika watafungwa jela.

Kwa mujibu wa Hailey ambaye taifa lake ni miongoni mwa ambayo hutoa ufadhili mkubwa humu nchini amesema mipango inayowekwa na serikali ya kitaifa vilevile za kaunti kufanikisha ugatuzi haiwezi kufaulu iwapo ufisadi utaendelea kukithiri na kuchangia uporaji wa mali ya umma.

Mwenyeji wa kongamano hilo la ugatuzi, Ann Waiguru aidha amezungumzia miradi mbalimbali liyofanikiwa kwenye kaunti yakekupitia ugatuzi ikiwamo afya akisema imeyaboresha pakubwa maisha ya wakazi.

Kwa upande wake, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi amesema anatarajia serikali ya kitaifa itatumia fursa ya kongamano hili kuweka wazi namna ajenda nne zitakavyofanikishwa ikizingatiwa zitatekelezwa kwenye kaunti.

Ikumbukwe ajenda hizo ni utoshelezo wa chakula, afya kwa wote, kubuniwa kwa nafasi zaidi za ajira kupitia kwa sekta ya viwanda na kujengwa kwa makazi yatakayokodishwa kwa bei nafuu.

Kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu kwa kiingereza ni Deliver, Transform, Measure, and Remain Accountable.

Related Topics

ugatuzi Nic Hailey