Mvutano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia Kujadiliwa

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni Balozi Monica Juma Alhamisi atafika mbele ya Kamati ya ulinzi ya Bunge la Kitaifa kuelezea zaidi kuhusu mvutano wa kidiplomasia baina ya Kenya na Somalia.

Juma ambaye jana alikuwa mbele ya Kamati hiyo, kuelezea kuhusu kiwango cha fedha alichotengewa katika wizara yake, katika bajeti ya mwaka huu, amesema mvutano huo, sio tu wa kidiplomasia lakini pia unahusu masuala ambayo ni muhimu kwa taifa hili.

Juma alikuwa akijibu maswali ya wanachama wa kamati hiyo waliotaka aelezee kwa kina kuhusu kiini hasa cha mvutano huo, na hatua ambazo serikali imechukua kuukabili.

Ikumbukwe Jumamosi iliyopita Kenya ilimfurusha Balozi wa Somalia humu nchini huku ikimwagiza Balozi wa Kenya nchini Somalia Luca Tumbo kurejea kwa mashauriano.

Kenya iliishtumu Somalia kufuatia hatua yake ya kupanga kunadi baadhi ya maeneo yenye mafuta na gesi kwenye eneo linalozozaniwa tarehe saba kwa kampuni kutoka mataifa ya Uingereza, Northern Ireland na Norway.

Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni Machari Kamau alisema hatua hiyo ilidhihirisha wazi kuwa haijakomaa kidipomasia.

Related Topics

Somalia