Ruto asema serikali itajadiliana na walimu kuhusu kodi ya nyumba ya asilimia 1.5

Serikali itajadiliana na walimu kuhusu mpango wa kuwatoza wafanyakazi wa umma kodi ya asilimia 1.5 ili kufanikisha utekelezaji wa mpango wa serikali wa ujenzi wa nyumba takriban laki tano ambazo zitakodishiwa wananchi kwa bei nafuu. Kauli hiyo imetolewa na Naibu wa Rais, William Ruto wakati wa kongamano la 20 la wajumbe wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri, KUPPET kufuatia malalamiko ya walimu kwamba huenda mpango huo ukawaathiri kiuchumi ikizingatiwa mapato yao bado ni ya chini.

Naibu wa Rais, William Ruto amesema lengo la kuwatoza walimu kodi hiyo ni kwa kuwa mradi huo unalenga kuwanufaisha Wakenya wote na kuhakikisha wanapata makazi bora.

Ruto alikuwa akiijibu kauli ya Katibu Mkuu wa KUPPET, Akelo Misori ambaye amesema ilivyo sasa baadhi ya walimu wanamikopo mingi walioomba ili kufanikisha mahitaji mbalimbali na iwapo watatozwa kodi hiyo huenda wakasalia bila chochote hivyo kulazimika kujihusisha na shughuli nyingine mbali na ualimu ili kukimu mahitaji yao.

Misori aidha amelalamikia suala la serikali kuchelewesha mpango wa kuwapandisha walimu vyeo hali ambayo inawafisha moyo baadhi yao katika utendakazi wao. Ameishtumu Tume ya Huduma za Walimu, TSC kwa kutokuwa na mpango dhabiti wa kuwapandisha walimu vyeo hali inayowafanya wengi kusalia katika kiwango kimoja kwa muda mrefu.

Mbali na hayo ameisihi serikali kuongeza idadi ya walimu katika shule za upili ikizingatia imeagiza kwamba watahiniwa wote waliofanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane, KCPE wajiunge na shule za upili.

Ruto amesema baadhi ya malalamishi yanayoibuliwa na walimu yanashughulikiwa na kuhimiza ushirikiano zaidi kati ya walimu na serikali ili kuafikiana namna ya kutimiza mahitaji yao.

Related Topics

KUPPET Ruto