ALIYEKUWA GAVANA WA NAIROBI EVANS KIDERO AMEHUSISHWA NA UFUJAJI WA SHILINGI BILIONI 21 ZA KAUNTI YA NAIROBI

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Evans Kidero ametuhumiwa kuchangia kupotea kwa shilingi bilioni 21 za serikali ya Kaunti ya Nairobi alipokuwa akihudumu katika wadhifa huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Uhasibu la KPMG iliyokabidhiwa Gavana wa sasa, Mike Sonko masuala kadhaa yameibuliwa kukiwamo kufunguliwa kwa akaunti kisiri, kuchukuliwa kwa kodi kutumia vitabu vya risiti ambavyo haviwezi kukaguliwa na matumizi ambayo yalifanywa pasi na kutumia mfumo rasmi wa serikali wa IFMIS.

Kwa mfano katika ripoti hiyo serikali ya Nairobi ilikuwa na akaunti 32 huku 13 zikikosa kutajwa wazi wakati wa kumkabidhi gavana Sonko mamlaka, mwaka uliopita. Takriban shilingi bilioni 21 zinasemekana kulipwa kupitia mifumo mingine pasi na ule rasmi wa serikali wa IFMIS.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya mwaka 2011 na mwaka 2017, Kaunti ya Nairobi ilitumia mifumo mbalimbali kukusanya fedha ukiwamo mifumo ya Ejijipay, IFMIS, Jumbo Link na Laiforms na hivyo kuwapo changamoto ya kujumuisha data kutoka  mifumo hii yote.

Vilevile katika ripoti hiyo, imebainika kwamba vitabu zaidi ya elfu 7 vilivyotumiwa na mawakala wa kaunti kukusanya kodi ya kuegesha magari vimeondolewa katika mfumo uliokuwa ukitumika huku ushahidi kuwa fedha hizo ziliwasilishwa kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi ukikosekana.

Ripoti hiyo imewasilishwa kwa Sonko na Mkuu wa Ushauri KPMG, Gerald Kasimu.