Utafiti mpya waonyesha kuwa Wakenya wengi hupenda kusafiri kifamilia

Wakenya wengi hupenda kusafiri kifamilia kuliko Wanaijeria ambao hupenda kusafiri kibinafsi, hii ni kulingana na utafiti mpya wa kampuni ya Jumia Travel.

Yani, huku asilimia 51 ikiwa ni usafiri wa kifamilia nchini Kenya, asilimia 6 ni usafiri wa kifamilia nchini Nigeria.

“Wakati huohuo, asilimia 13 ya Wakenya hupenda kusafiri kibinafsi, ikilinganishwa na asilimia 65 ya Wanaijeria,” inaelezea sehemu ya ripoti ya Jumia Travel iliyozinduliwa rasmi Jumatano.

Isitoshe, akisomea wanahabari matokeo ya utafiti huo, Meneja wa Jumia Travel, Cyrus Onyiego, alikuwa na haya ya kusema:

“Nchini Kenya, asilimia 64 ya wanaume hulala hotelini ikilinganishwa na asilimia 78 nchini Nigeria.

Kwa upande mwingine, asilimia 36 ya wanawake nchini hulala hotelini ikilinganishwa na asilimia 22 nchini Nigeria.”

Picha nyingine inayojitokeza kutoka ripoti ya Jumia Travel ni kwamba, humu nchini, asilimia 43 ya wasafiri ni wa umri wa miaka 35 hadi 54 ambayo ni idadi kubwa ikilinganishwa na asilimia 40 ya wasafiri wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 34, pamoja na asilimia 6 ambao ni wasafiri wenye umri wa miaka 18 hadi 24.

“Nchini Nigeria, asilimia 4 ni idadi ya wasafiri wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 24, huku asilimia 38 ni wasafiri wa miaka 25 hadi 34.

Tena huko huko Nigeria, asilimia 53 ya wasafiri ni wenye umri wa kutoka miaka 35 hadi 54,” akasema Bw Onyiego.

Akimalizia, Meneja huyo pia aliguzia kuwa Wakenya wenyewe ndio husafiri maeneo ya nchini kwa idadi kubwa (asilimia 59) ikilinganishwa na asilimia 41 ya wasafiri wa mataifa mengine.

“Lakini wasafiri hao hufurika mji wa Mombasa (asilimia 30); Nairobi (asilimia 29); Naivasha/Nakuru (asilimia 17); Mlima Kenya (asilimia 6); Kisumu (asilimia 5); Eldoret (asilimia 3); sehemu zingine (asilimia 7),” akasema Onyego.

Related Topics

Usafiri Kenya