CORD wawataka wabunge kupitisha ripoti kuhusu IEBC

Na,Carren Omae
Kwa mara nyingine Muungano wa CORD umeyahimiza mabunge ya Kitaifa na Seneti kujadili na kupitisha ripoti ya kamati ya pamoja iliyoshughulikia suala kuhusu hatima ya makamishna wa IEBC, bila kuifanyia marekebisho. Kwenye mkutano wa dharura na magavana pamoja na wabunge wa mrengo huo ulioongozwa na Kinara wao Raila Odinga, imeafikiwa kwamba watashirikiana na muungano wa Jubilee kufanikisha marekebisho kwenye Tume ya Uchaguzi IEBC na kwamba ripoti hiyo itapitishwa bila kufanyiwa marekebisho yoyote.
Kauli hiyo ya Raila vilevile imeungwa mkono na vinara wenza, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula, ambao wamesema kuandaliwa kwa ripoti hiyo ni mwanzo wa kukabili changamoto za uchaguzi, kama vile wizi wa kura. Wamesema ni sharti mapendekezo hayo yaanze kutekelezwa mara moja baada ya kupitishwa na bunge kuhakikisha uchaguzi mkuu haucheleweshwi.
Mkutano huo umeandaliwa huku baadhi ya wabunge wa ODM wakimlaumu Seneta James Orengo kwa kutoushinikiza ipasavyo upande wa Jubilee katika kamati ya pamoja kuhusu mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, hivyo kuupa usemi zaidi kwenye maafikiano hayo yatakayojadiliwa bungeni leo hii.
Miongoni mwa maafikiano hayo ya wiki jana ni kuwa Rais Uhuru Kenyatta atakabidhiwa orodha ya majina ya watu kumi na mmoja na kuwateua makamishna saba watakaohudumu katika tume hiyo ya uchaguzi.