Wahudumu wa afya waapa kuendelea na mgomo

Na Mike Nyagwoka

Kufuatia mgomo wa wahudumu wa afya unaoendelea, serikali sasa imependekeza kuwapa madaktari nyongeza ya shilingi elfu 36 kwa wanaohudumu daraja ya L huku walio na daraja ya M wakipendekezwa nyongeza ya shilingi elfu 42.
Kwenye nyongeza hii ambayo tayari imekataliwa na  Katibu Mkuu wa KMPDU, Ouma Oluga, Daktari anayelipwa chini zaidi angetarajia  kupata kati ya  shilingi elfu 176  na shilingi elfu 186 huku  wanaolipwa juu zaidi wakipata kati ya shilingi lefu 450 na shilingi 560. Nyongeza hii imependekezwa kwa kigezo kwamba madaktari warejee kazini huku marupurupu mengine yakiendelea kujadiliwa kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini mwaka 2013. Hata hivyo,  huku akikiri kuwa mgomo unaoendelea umewasababishia wakenya masaibu si haba, Oluga ameilaumu serikali kwa kutotimiza ahadi yake ndiposa wanagoma. Aidha, kwa mujibu wa Oluga, serikali ina mpango wa kuwafuta kazi baadhi yao jambo ambalo wamesema halitawatisha kamwe.
Hayo yanajiri huku mgomo huo ukichukua   mkondo mwingine, baada maafisa wa afya chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Nairobi wanaotoa huduma za afya katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kusema kwamba watajiunga na wenzao wanaogoma. Maafisa hao wamesema watalazimika kusitisha huduma zao katika hospitali hiyo iwapo hakutakuwa na maafikiano kati ya serikali na wahudumu wa afya.
Ikumbukwe tayari madaktari wamezitaka hospitali za binafsi na zile za Kimishonari kutotoa huduma zao kuanzia siku ya Jumanne ili kuishinikiza serikali kutekeleza mkataba wa mishahara uliotiwa saini mwaka 2013.
Hata hivyo licha ya mgomo huo, baadhi  hospitali katika Kaunti  za Bomet na Meru zingali zinahudumu kufutia maafikiano baina ya serikali na wahudumu wa afya. Katika Kaunti ya Nakuru, serikali ya kaunti imelazimika kuwaajiri wauguzi zaidi na kufungua baadhi ya hospitali ili kuendelea kuwahudumia wakazi.