Wario Abuni Jopo maalum kuchunguza madai ya Usimamizi mbaya, Rio

Na,Suleiman Yeri
Waziri wa Michezo, Hassan Wario amebuni jopo maalum la kuchunguza madai ya usimamizi mbaya wakati wa michezo ya Olimpiki jijini Rio Brazil.
Kamati hiyo ya makamishna wanane imejukumiwa kuchunguza masuala mbalimbali kukiwamo kupotea kwa jezi rasmi za wanariadha, idadi kamili ya wanariadha waliosafiri na orodha iliyoidhinishwa na Kamati ya Olimpiki Nchini, NOCK.
Kamati hiyo itakayoongozwa na DKt. Paul Ochieng ina siku thelathini kuhakikisha inafanya uchunguzi huo na kuwasilisha ripoti yake.
Wanachama wengine wa kamati hiyo ni Rose Tatamuya atakayekuwa Naibu Mwenyekiti, Elizabeth Olaba, Moses Kiptanui, Hussein Kipkemboi, Mwanahabari Elias Makori, Wakili Njeri Onyango na afisa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Wakati uo huo, Wario amesema Kenya imeionesha dunia kuwa taifa hili halitumii dawa za kusisimua misuli.