Rais Uhuru Kenyatta apongezwa kwa uongozi bora

Na, Sophia Chinyezi

Viongozi wa Taasisi za Fedha wa mataifa mbalimbali ulimwenguni wamempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa mtazamo na uongozi bora ambao wanasema ni muhimu katika ukuaji wa bara la Afrika. Haya yanajiri huku Kongamano la Sita la Kimataifa la Tokyo Kuhusu Ustawi wa Bara Afrika TICAD, likianza.
Kiongozi wa Benki ya Dunia na African Development Bank, AFDB amesema sera za Kenya zilizoanzishwa na Rais Kenyatta zimeweka mazingira mazuri ambayo yamechangia uwekezaji, biashara kati ya mataifa ya Afrika, vilevile kuiwezesha Kenya kuwa miongoni mwa mataifa ambayo yameimarika pakubwa.
Akihutubu mapema leo katika Ikulu ya Nairobi alikokutana na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, Uhuru ameelezea imani yake kuwa kongamano hilo litaimarisha biashara, kujadili changamoto zinazowakumba Waafika pamoja na kuimarisha umoja barani humu.
Wajumbe zaidi ya elfu kumi, wakiwamo marais wa mataifa thelathini na matano wanahudhuria kongamano hilo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano, KICC litakalokamilika Jumapili wiki hii.