JSC haitaweka wazi taratibu zilizotumika kuwateua watakaowania wadhifa wa Jaji Mkuu

NA, SOPHIA CHINYEZI

JSC haitaweka wazi taratibu zilizotumika kuwateua watakaowania wadhifa wa Jaji Mkuu

Tume ya Huduma za Mahakama JSC imekataa ombi la kuwataka kuweka wazi taratibu zilizotumika kuwateua watakaowania wadhifa wa Jaji Mkuu. JSC imeiambia mahakama kwamba baadhi ya walionyimwa nafasi kuwania wadhifa huo walipokea barua kutoka kwao kufafanua taratibu zilizofuatwa.
Kwenye barua iliyowasilishwa mahakamani, JSC vilevile imesema walioteuliwa waliafikia vigezo zilivyohitajika kwa mujibu wa katiba. Wakili anayeiwakilisha tume hiyo, Njoroge Regeru amesema kuna haja ya nafasi zilizoachwa; yaani ya Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na Jaji wa Mahakama ya Juu, kujazwa haraka iwezekanavyo, na kuongeza kuwa kuteuliwa kwa watakaojaza nyadhifa hizo ni muhimu kwa umma. Regeru ndiye aliyeiwasilisha barua hiyo mahakamani.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Katiba, Yash Pal Ghai aliilaumu tume hiyo kwa kuwanyima wananchi taarifa muhimu kuhusu walivyoafikia orodha ya walioteuliwa. Ameilaumu JSC kwa kushindwa kuongoza katika kufanikisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa haki.
Jumla ya watu sita wameorodheshwa kujaza nafasi ya Jaji Mkuu iliyokuwa ikishikiliwa na Willy Mutunga ambaye alistaafu mapema. Wanawake kumi na watatu waliteuliwa kwa wadhifa wa Naibu Jaji Mkuu, ambao ulikuwa ukishikiliwa na Kalpana Rawal, aliyestaafu akiwa na miaka sabini.